Home » » ADC YATISHIA KUMSHITAKI DC

ADC YATISHIA KUMSHITAKI DC


na Sitta Tumma, Mwanza
SAKATA la kuchomwa moto kwa makazi ya watu 300 wilayani Magu, Mwanza, limeanza kuchukua sura mpya, baada ya Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), kutangaza kusudio la kumshtaki Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Jackline Liana, kwa madai ya kuvunja sheria zikiwemo haki za binadamu.
Chama hicho kimesema tayari kimeanza kuwasiliana na wanasheria wake kwa ajili ya kukusanya ushahidi, kisha kufungua kesi ya madai mahakamani, kwani kitendo kilichofanywa na Serikali ya Magu ni unyama na uonevu wa hali ya juu.
Kamishna wa chama hicho Kanda ya Ziwa, Shaban Itutu, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusiana na tukio hilo lililotokea kati ya Julai 31 na Agosti Mosi, mwaka huu.
Alisema chama hicho kinalaani kitendo hicho na kwamba hawatakivumilia, kwani kinavunja haki za binadamu na sheria za nchi.
“Kitendo cha serikali kuteketeza kwa moto makazi ya watu ni unyama mkubwa. Pia ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu... kwa hiyo chama cha ADC tumeanza kuzungumza na wanasheria wetu kwa ajili ya maandalizi ya kuandaa kesi.
“Serikali inaposema wananchi hawa wamevamia hifadhi ya wanyamapori siyo kweli. Hawa watu wameanza kuishi maeneo hayo mwaka 1913 kabla ya vita ya pili ya dunia, na serikali imetoa hadhi ya hifadhi mwaka 1992. Sasa nani aliyemkuta mwenzake?” alihoji kamishna huyo.
Katika tukio hilo, inadaiwa Mkuu wa Wilaya ya Magu akiwa na maofisa wa serikali, wakiwemo wa Jeshi la Polisi alisimamia zoezi la kuchomwa na kuteketeza kwa moto kaya 55 zenye nyumba 90 zilizokuwa na zaidi ya wakazi 300, wanaodaiwa kuvamia hifadhi ya wanyamapori ya Sayaka.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa