Tone

Tone
Home » » RIDHIWANI KIKWETE KUONGOZA HARAMBEE MWANZA

RIDHIWANI KIKWETE KUONGOZA HARAMBEE MWANZA


Bw.Ridhiwani Kikwete
MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan Kikwete, anatarajiwa kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha Afya katika Kata ya Ng'hungumalwa Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza, ambapo zaidi ya sh. milioni 150 zinahitajika.

Katika harambee hiyo, Ridhiwan ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Baraza la Vijana la Chama cha Mapinduzi (UVCCM), ndiye atakayekuwa mgeni rasmi, ambapo wageni mbali mbali wakiwemo viongozi wa vyama na Serikali kutoka Mikoa ya Tabora, Mwanza, Shinyanga, Geita na Mara watahudhuria harambee hiyo itakayofanyika Aprili 14 mwaka huu.

Mwandishi wa mtandao huu kutoka Mwanza, Sitta Tumma anaripoti kwamba; Akizungumza jana kwenye kikao cha ufanikishaji wa harambee hiyo, kilichofanyika Hungumalwa mjini, Diwani wa Kata hiyo ya Ng'hungumalwa, Shija Malando (CCM), alisema fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo zitatumika kukamilisha jengo la Kituo cha Afya, ambalo kwa sasa limejengwa hadi kwenye lenta.

"Tunahitaji zaidi ya sh. milioni 150 katika harambee hii. Fedha hizi zitasaidia kumalizia ujenzi wa kituo chetu cha afya. Tunaamini ujio wa Ridhiwan utavuka lengo la fedha halisi tunazohitaji.

"Kukamilika kwa kituo hiki cha afya, itasaidia sana kuondoa kero kubwa inayowakumba wananchi wa kaya hii ya Ng'hungumalwa. Hadi sasa kata hii haina Zahanati wala kituo cha afya, tunaomba Mungu malengo yetu yafanikiwe", alisema diwani Malando.

Hata hivyo, Malando ambaye anaonekana kutekeleza vema ahadi zake kwa wananchi wa Hungumalwa, alisema hadi sasa wananchi wa kata yake hiyo wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilometa 40 kufuata huduma za afya, huku wengine wakishindwa kumudu gharama za usafiri kufuata huduma hizo ambazo si chini ya 200,000.

Kwa mujibu wa diwani huyo kijana ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, wagonjwa wakiwemo akina mama na watoto wamekuwa wakilazimika kusafiri hadi mkoani Shinyanga, Ngudu na wengine kwenda Wilayani Misungwi kufuata huduma, jambo ambalo ni kero kubwa.

Awali, mwenyekiti wa kamati ya ufanikishaji wa harambee hiyo, Michael Machenje alisema, upatikanaji wa kituo hicho cha afya ni mikakati maalumu ya kuwaondolea wananchi kero kubwa wanayoipata kwa sasa katika ukosefu wa huduma za kitabibu karibu yao.

"Tumeona Serikali haiwezi kutufanyia kila kitu, ndiyo maana tumeamua kuitisha harambee hii na kumwalika mtoto wa Rais, Ridhiwani aje atuchangishie. Tunaamini tutavuka lengo", alisema mwenyekiti huyo wa kamati ya ufanikishaji, Machenje.

Katika kikao hicho, wajumbe wa kamati hiyo ya ufanikishaji wa harambee walihimizana kutoa michango yao ambapo kila mmoja anatakiwa achangie sh. 20,000 kabla siku ya harambee haijafika, na kwamba wajumbe wengi walishachanga na baadhi wameahidi kukamilisha michango yao mwishoni mwa wiki hii.

Ilielezwa kwamba, ujenzi wa kituo hicho cha afya Ng'hungumalwa, kitapunguza pia vifo vya wagonjwa wanaopoteza maisha kwa kukosa huduma kwa wakati, na kwamba kitawasaidia maradufu wananchi wakiwemo wajawazito, watoto na watu wote watakaokuwa wakihitaji huduma za kitabibu katika eneo hilo.
Kwa hisani ya Francis Godwin 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa