WANANCHI MWANZA WAMETAKIWA KUSHIRIKI ZOEZI LA UBORESHAJI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

Wananchi wa mkoa wa Mwanza wametakiwa kushiriki zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda wakati wa hafla ya kilele cha maonesho ya kilimo nane nane katika viwanja vya Nyamhongolo vilivyopo Manispaa ya Ilemela.

" Ni haki na wajibu wa kila mtanzania alie na vigezo vya kupiga kura kujiandikisha na kupiga kura ili kupata viongozi tunaowataka." Amesema Mhe. Mtanda

Aidha ameongeza kuwa ni lazima viwanja vya Nyamhongolo kufanyiwa maboresho,kuwa na miundo mbinu ya kudumu ili kuleta hamasa zaidi kwa washiriki na kuboresha ulinzi na usalama wa mali za washiriki.

Kabla ya hafla hiyo Mhe.Mtanda alipata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda kujionea bidhaa na vipando vya mazao mbalimbali.

"Banda la Manispaa ya Ilemela limekuwa la tofauti limetufundisha kilimo cha mijini,kilimo kinachotumia nafasi ndogo na kuleta tija kubwa."

Mhe.Mtanda amemkabidhi kikombe cha ushindi wa nafasi ya pili Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi. Ummy Wayayu  kwa Manispaa yake katika  kundi la taasisi za serikali za mitaa.

Akihitimisha maonesho hayo Mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Maonesho ya kanda ya ziwa magharibi yamejumuisha mikoa miwili ya Mwanza na Geita huku yakipambwa na kauli mbiu isemayo chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo,uvuvi na ufugaji.

 


RC MTANDA AHIMIZA WELEDI KWA WAKANDARASI WAZAWA MIRADI YA SERIKALI,AZITAKA TAASISI KUJENGA VIWANJA VYA MICHEZO




Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda leo Agosti 5,2024 amefanya ziara fupi ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar-e-s Salaam Tawi la Mwanza unao gharimu shs bilioni 37 unatekelezwa na Mkandarasi mzawa Kampuni ya Comfix Engineering na kuhimiza weledi katika miradi ya Serikali.

Mkuu huyo wa Mkoa akiwa na mkurugenzi wa tawi hilo Dkt.Albert Mmari amejionea hatua ya umaliziaji wa majengo manne ya ufundishaji,Taaluma na hosteli za wanaume na wanawake pamoja na uwanja wa michezo wa siku nyingi wa tawi hilo na kutaka uboreshwe ili uje kuwa na tija zaidi.

"Nimefurahishwa na uwanja huu na hapa naomba nitoe msisitizo,Taasisi zote za Serikali na binafsi jengeni viwanja vya michezo nchi yetu ipo mbioni kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON 2027 na huenda CCM Kirumba ukatumika mtajiongezea vipato timu zikija kufanya mazoezi,"amesisitiza Mtanda.

Amesema katika michuano ya ligi kuu ya NBC timu mbalimbali zitafika kucheza na Pamba Jiji FC na wakati zinajiandaa na mechi zitahitaji viwanja vya mazoezi.

Akizungumza kampuni za watanzania kupewa miradi mikubwa ya Serikali,Mtanda amesema ni wajibu wao kutanguliza uaminifu na kuikamilisha kwa wakati hali ambayo itawajengea kuaminiwa na Serikali.

"Huu mradi wa miundombinu hii uliogharimu fedha nyingi ni mfano mzuri kwa mkandarasi huyu,kila jengo naambiwa linakamilika mwaka huu,endeleeni na weledi huu,"Mtanda

Kwa upande wake mkurugenzi wa tawi hilo Dkt.Albert Mmari amesema ujenzi huo una malengo makuu matatu kuongeza udahili,kuongeza programu ya elimu ya ufundi na ushirikiano wa kikanda.

"Mara baada ya mradi huu kukamilika utakuwa na tija kwa nchi za Afrika Mashariki na kati kwa watu kuja kupata utaalamu wa juu namna ya kuzalisha bidhaa za ngozi,"Dkt.Mmari

Ujenzi huo wa majengo ya kisasa ulioanza mwaka 2019 na utakamilika mwaka huu.

WATAALAM WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUFANIKISHA AJENDA YA LISHE MASHULENI


Wataalam wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wametakiwa kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha ajenda ya lishe inatekelezeka na kufanikiwa katika shule zote za manispaa hiyo.

Rai hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela Dkt.Maria Kapinga wakati akizungumza na watendaji wa kata,mitaa na maafisa elimu kata katika ukumbi wa jengo jipya la utawala ambapo amefafanua kuwa ili suala la lishe mashuleni liweze kufanikiwa ni lazima wataalam hao waunganishe nguvu kwa pamoja kwa kuishirikisha jamii .

‘.. Ajenda ya lishe ni ajenda ya Mheshimiwa Rais, kwa hiyo sisi sote tuna jukumu la kuhakikisha ajenda hii inafanikiwa na watoto wanakuwa na afya bora, kuanzia wale wachanga mpaka wanafunzi wale wa mashuleni, mtoto hawezi kuwa na uwezo mzuri wa kufikiri kama afya yake ni dhaifu ..’ Alisema

Aidha Dkt.Kapinga amewahakikishia ushirkiano wataalam wote wa sekta nyingine kwa muda wote wataohitaji kufanya hivyo ili kuhakikisha zoezi la lishe mashuleni linafanikiwa .

Mwl.Marco Busungu ni Afisa elimu msingi Manispaa ya Ilemela yeye amewataka wataalam hao kujituma na kutanguliza uzalendo katika kutekeleza majukumu yao kuhakikisha masuala ya lishe  yanafanikiwa na kwamba kwa mwaka huu wa fedha zipo jitihada ambazo serikali imezichukua katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya uratibu wa shughuli za lishe kwa watendaji wa mitaa na kata .

Nae Mratibu wa lishe Manispaa ya Ilemela Bi.Pili Khasimu amesema kuwa Tanzania ilianzisha siku ya afya na lishe ya kijiji katika miaka ya 1980 ikilenga kuongeza ufuatiliaji wa lishe ukuzaji wa viwango vya vituo vha afya katika kutoa huduma kwa kuongeza elimu ya unyonyeshaji, chanjo, matumizi ya Oral Rehydrated Salt (ORS) na uanzishaji wa chakula cha nyongeza.

 Ameongeza kuwa tangu mwaka 2023 wadau tofauti nchini wameijumuisha siku ya afya na lishe ya kijiji au mtaa kama sehemu muhimu katika program zao ambazo zimeonekana kuwa nzuri katika kutoa huduma kamili za maendeleo ya awali ya mtoto pamoja na huduma za lishe katika ngazi ya jamii.

Wakichangia kwa nyakati tofauti Kelvin Gilo ambae ni mtendaji wa mtaa wa Igumamoyo kata ya Sangabuye na Asha Mahiza ambae ni Afisa elimu kata ya Nyakato wameshauri kutengwa kwa bajeti toshelezi kwa ajili ya  kufanikisha shughuli zote za lishe ikiwemo uelimishaji sambamba na mchakato wa kutunga sheria ndogo itakayosimamia masuala ya lishe.

 

JAMII YATAKIWA KUACHA DHANA POTOFU DHIDI YA UNYONYESHAJI

Jamii imetakiwa kuacha dhana potofu dhidi ya unyonyeshaji ili kuwafanya watoto kuwa na afya njema na kukua vizuri kimwili na kiakili.

Hayo yamebainishwa na mwakilishi wa mganga mkuu wa manispaa ya Ilemela Dkt. Barnabas G. Mwaikuju  wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama duniani yaliyofanyika katika viwanja vya kituo cha Afya Buzuruga ambapo amekemea imani na fikra potofu zinazochangia kukwamisha unyonyeshaji wa watoto ikiwemo kuamini watoto wasiponyonya mama atabaki kuwa binti, kuwanywesha watoto maji badala ya kunyonya wakiamini kila mtoto anapolia anakuwa na kiu hivyo kushauri kuzingatia ushauri wa wataalam katika kunyonyesha watoto kwa ufasaha.

‘.. Kunyonyesha mtoto ni msingi bora wa ukuaji wake,huimarisha viungo na akili..' Alisema

Aidha Daktari Mwaikuju amewasisitiza wazazi na walezi kuhudhuria katika vituo vya kutolea huduma za afya pindi zinapojitokeza changamoto wakati wa unyonyeshaji badala ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji na watu wengine wasiokuwa na utaalamu.

Nae Bi. Pili Kasimu ambae ni mratibu wa lishe kwa manispaa ya Ilemela amewataka wa mama kuzingatia lishe za watoto ili kuwakinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo mdomo wazi, kichwa kikubwa pamoja na kutumia dawa za kuongeza damu na si kuzitupa.

Damarice Dawson ni muuguzi katika kituo cha Afya Buzuruga ambapo amewaonyesha wazazi waliohudhuria katika maadhimisho hayo namna bora ya kunyonyesha watoto pamoja na kuzingatia mkao, namna ya kuwabeba na kuwashika ili watoto waweze kunyonya kwa urahisi.

Anna Boniphace na Joanita Philipo ni wananchi kutoka mitaa ya Nyambiti na Buzuruga ambapo wameshukuru kwa elimu iliyotolewa huku wakiahidi kuizingatia na kuifanyia kazi ili watoto wao wakue vizuri pamoja na kuwaelimisha wananchi wengine.

Wiki ya maadhimisho ya unyonyeshaji maziwa ya mama hufanyika kila mwaka Agosti 1-7,  kwa mwaka huu imebebwa na kauli mbiu ya ‘Tatua changamoto, Saidia unyonyeshaji kwa watoto’ huku kwa ilemela ikiadhimishwa kwa kutoa elimu na kuhamasisha juu ya unyonyeshaji katika vituo vyote vya kutolea huduma na katika jamii kupitia maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya mtaa (SALIM).

 

BILIONI 1.2 KUJENGA SHULE MBILI ZA SEKONDARI NA NYUMBA

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imepokea jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 1,268,560,418.00 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za sekondari, Masemele sekondari katika kata ya Shibula na Kilabela sekondari katika kata ya Bugogwa pamoja na ujenzi wa nyumba moja ya walimu katika shule ya sekondari Kisenga iliyopo kata ya Kiseke.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi.Ummy Wayayu wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli zilizotekelezwa na ofisi yake katika mkutano wa baraza la madiwani kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo amefafanua kuwa ujenzi wa kila shule utagharimu kiasi cha shilingi Milioni 584.2 sambamba na ujenzi wa nyumba moja kwa gharama ya shilingi Milioni 100 itakayogawanyishwa mara mbili “2 in 1” kwa ajili ya waalimu wawili kuishi.

“ Fedha hizi zilipokelewa mwishoni mwa mwaka wa fedha uliopita na taratibu za kutambua maeneo ujenzi utakakofanyika zinaendelea na tunatarajia utekelezaji wake utakamilika mara moja .”

Aidha Bi. Wayayu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya manispaa yake huku akiwaomba viongozi wenzake kuendelea kushirikiana katika kusimamia matumizi bora ya fedha hizo kwenye maeneo yao.

Nae Mbunge wa Ilemela Mhe.Dkt.Angeline Mabula mbali na kumpongeza Mkurugenzi huyo kwa taarifa nzuri ya utekelezaji amesema kuwa serikali kupitia ombi lake bungeni  imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya ufundi itakayojengwa kata ya Bugogwa na shule mpya ya msingi itakayojengwa kata ya Shibula na kuwaomba madiwani kushirikiana katika maendeleo.

“ Wataalam wetu naomba muanze kuwaza ujenzi wa shule za ghorofa ,ardhi haiongezeki ila watu wanaongezeka .” Amesema mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga.

Diwani wa kata ya Nyakato Mhe.Jonathan Mkumba amepongeza taarifa ya Mkurugenzi iliyoonyesha mgawanyo mzuri wa fedha katika kila kata kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo.

Sarah Shija ni mkazi wa mtaa wa Buswelu ni mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa baraza la madiwani yeye anapongeza jitihada za uboreshaji wa miundo mbinu ya elimu inayofanywa na serikali.

 

RC MTANDA AKUTANA NA UONGOZI WA MADEREVA WA SERIKALI ,AWAAHIDI MAZINGIRA BORA YA KAZI

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda leo Agosti 2,2024 amekutana na uongozi wa madereva wa Serikali mkoani humo na kuwaahidi mazingira mazuri ya kazi hasa maslahi yao

Mazungumzo hayo mafupi yaliyofanyika Ofisini kwake Mkuu huyo wa mkoa amesema  kazi siku zote ili zifanikiwe ni lazima kuwepo na hali ya kutegemeana na siyo kubaguana.

"Mmefanya vizuri kunipa ulezi wa chama chenu ni eneo ambalo nitalitendea vizuri kwa uzoefu nilionao,nitahakkikusha magari yote yanafufuliwa na yaliyo hatua ya kuuzwa yafanyiwe hivyo,amesisitiza Mtanda

Amewataka madereva kuyatunza magari ya Serikali na kutosita kutoa ushauri wa kiufundi inapo bidi kwa wakubwa wao ili vyombo hivyo viendelee kudumu na kuepuka hasara kwa Serikali.

Aidha amezitaka Taasisi zote za Serikali pamoja na Halmashauri kuhakikisha zinawapa ruhusa madereva wao kuhudhuria mkutano wao mkuu utakaofanyika kuanzia Agosti 18 hadi 23 mwaka huu Jijini Arusha na kufunguliwa na Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa

Mwenyekiti wa chama cha madereva wa Serikali  mkoani Mwanza Enock Jeremia amemuhakikishia mkuu huyo wa mkoa kiyazingatia maelekezo yote aliyowapa.


 

KAMPENI YA PAMBA DAY YAZIDI KUPAMBA MOTO,TAWI LA WANACHAMA LAFUNGULIWA BUCHOSA

Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya siku inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka Jijini Mwanza,Pamba Day,kampeni yake imezidi kuwabamba mashabiki baada ya kufunguliwa tawi jipya huko Buchosa wilayani Sengerema.

Tawi hilo la mashabiki wa Pamba Jiji FC limefunguliwa leo Agosti Mosi,2024 na katibu Tarafa wa kata ya Kahunda,Joseph Kapunda kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo na kusisitiza huo ni muendelezo wa kufunguliwa matawi zaidi  wilayani humo.

"Tuna wajibu wa kushikamana kwa vitendo kuiunga mkono timu yetu ya Pamba Jiji FC ambayo mbali na burudani imekuja kuinua uchumi wa mkoa wetu,"Kapunda.

Amesema siku ya Pamba Day itadhihirisha furaha ya mashabiki kwa timu yao kwa kuujaza kwa wingi uwaja wa CCM Kirumba na mechi zote za ligi kuu ya NBC.

"Tulimsikia Mkuu wetu wa Mkoa Mhe Said Mtanda akituhimiza kushikamana na tuwe wachezaji wa 12 uwanjani siku zote za michuano ya timu ya Pamba Jiji akimaanisha kuishabikia uwanjani",amesisitiza katibu Tarafa wakati akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa tawi la mashabiki wa Pamba Jiji FC.

Mwenyekiti mteule wa tawi hilo Salawe Magembe                      amebainisha atahakikisha kwa kushirikiana na wanachama wenzake wanazidi kuliimarisha tawi hilo na kuwa wakereketwa wa kweli kwa timu ya Pamba Jiji FC

Mchezaji wa zamani wa Pamba miaka ya 90 ambaye alikuwa mlinda mlango Madata Lubigisa amewataka mashabiki wa soka kuhakikisha timu yao inadumu katika ligi hiyo na kuwa tishio kwa timu za uzito wa juu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

"Nimefurahi mlivyo hamasika na timu yenu ya Wana Kawekamo TP Lindanda,Pamba Jiji FC ufunguzi wa tawi hili uwe msingi bora wa kupanga mikakati mbalimbali ya kuipa maendeleo timu yenu,"Agnes Magubu,kiongozi wa Kampeni ya Pamba Day

Kampeni hiyo inayoendelea kwenye wilaya zote za Mkoa wa Mwanza inakwenda Pamoja na uuzwaji wa tiketi za kuingilia siku ya Pamba Day na jezi za timu hiyo.



 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa