WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema kuwa ni vigumu
kuuondoa umaskini nchini kama serikali haitaongeza uuzaji wa bidhaa
zake nje ya nchi.
Alisema serikali pia lazima ivilinde viwanda vyake vichanga dhidi ya ushindani wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje.
Wito huo aliutoa jana mkoani Mwanza, wakati akitoa mada ya ‘Ujenzi na
Ukuzaji wa Uchumi Imara’ katika mkutano wa Wanafunzi wa Chuo cha
Elimu ya Biashara (CBE).
Alisema ongezeko la ajira na ukuaji wa uchumi utategemea sana na
jinsi nchi husika itakavyouza nje bidhaa kutoka viwanda vyake hivyo ni
vema serikali ikatoa ulinzi katika sekta binafsi.
“Nchi inatakiwa iuze zaidi nje kuliko inavyoagiza kutoka nje kwa nchi
zetu maskini, hali hii ni kinyume kabisa, ndiyo maana umaskini
hauishi,” alisema.
Alisema baadhi ya nchi za nje zimekuwa zikitoa upendeleo wa
kisirisiri kwa bidhaa zao wanazopeleka nje ya nchi, jambo linalofanya
uwepo ushindani usio halali kwa soko la ndani.
Aliongeza kuwa kigezo kimojawapo muhimu kinachotofautisha nchi
zilizoendelea na zinazoendelea ni uwepo wa viwanda vinavyozalisha
bidhaa za kuuzwa katika soko la dunia.
Sumaye alisema kwa ukuaji endelevu wa uchumi lazima Tanzania ijenge
na kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za viwandani ili ziwe na ubora na
wingi unaotosheleza ushindani katika masoko ya nje.
“Tunahitaji utaalamu wa teknolojia za kisasa katika uzalishaji,
rasilimali watu wenye utaalamu na ujuzi wa kutosha, zana za kisasa za
uzalishaji na ujuzi wa masoko,” alisema.
Sumaye alisema nchi za Afrika zinapaswa kutunga sera rafiki kwa
maendeleo ya sekta binafsi na kulinda sekta changa isiuawe na ushindani
usio halali kutoka nje.
“Ni lazima kuwe na sera ya makusudi ya kuongeza uuzaji nje wa bidhaa na huduma kama tunataka kujenga utajiri ndani ya nchi.
“Uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi hujenga utajiri kwa kuuza
bidhaa na huduma zake katika masoko ya nje. Hii ndiyo maana uwiano wa
biashara ni muhimu sana,” alisema.
Alibainisha kuwa sekta binafsi kama kiongozi wa maendeleo ya uchumi
endelevu ichukue nafasi yake na serikali ishirikiane nayo badala ya
kuiona ni mshindani au adui kwake.
Sumaye alisema usindikaji wa kubadilisha bidhaa za mazao kuwa bidhaa
za viwandani ndio mfumo unaotumiwa na mataifa yaliyoendelea wakati nchi
nyingi zinazoendelea duniani hutegemea kilimo ambacho hushindwa
kuyaongezea thamani mazao yanayozalishwa.
Alibainisha kuwa mazao yasiyoongezwa thamani yoyote hununuliwa kwa
bei za chini na isiyotabirika, hivyo kuzifanya nchi maskini kupoteza
sehemu kubwa ya biashara zao katika soko la kimataifa.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
1 comments:
Amakweli kila shabiki ni mjuzi kuliko kila mchezaji.Huyu mweshimiwa alipokuwa kwenye nafasi yake alikuwa hayaongelei haya, leo hii kawa mkosoaji na mshauri mkubwa!duu
Post a Comment