Home » » AGPAHI YATOA MAFUNZO YA HUDUMA ZA KISAIKOLOJIA KWA WAHUDUMU WA VITUO VYA TIBA NA MATUNZO MWANZA

AGPAHI YATOA MAFUNZO YA HUDUMA ZA KISAIKOLOJIA KWA WAHUDUMU WA VITUO VYA TIBA NA MATUNZO MWANZA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi mkoa wa Mwanza Dk. Pius Masele.
***
Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limeendesha mafunzo kuhusu msaada na huduma za kisaikolojia kwa wahudumu wa jamii wanaosaidia kazi katika vituo vya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) vilivyopo katika halmashauri za wilaya mkoani Mwanza.
Mafunzo hayo ya siku tano yanayokutanisha wahudumu wa jamii kutoka halmashauri za wilaya za Ilemela,Kwimba, Magu,Buchosa,Misungwi,Sengerema na Nyamagana yanafanyika kuanzia Jumatatu Februari 12,2018 hadi Ijumaa 16 Februari ,2018 katika ukumbi wa Midland Hotel jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi mkoa wa Mwanza Dk. Pius Masele alisema mafunzo hayo yatawasaidia watoa huduma ngazi ya jamii kuboresha huduma katika vituo vya afya kwenye maeneo yao.
“Kupitia mafunzo haya mtaweza kuwaunganisha wateja na huduma mbalimbali za kijamii ili kuhakikisha kunakuwepo uendelevu wa huduma kwenye vituo vya tiba na matunzo ikiwa ni pamoja na kuwarudisha kwenye huduma wateja waliopotea”,alisema Dk. Masele.
“Naomba mkafuatilie wateja waliopotea, muwaelimishe kuzingatia ufuasi mzuri wa dawa na kuhakikisha hawapati maambukizi mapya na magonjwa nyemelezi kwani hatutaki kuona mgonjwa anakuwa wa kulala kitandani, sisi tunataka watu washiriki katika shughuli za maendeleo”,aliongeza Dk. Masele.
Aidha alilishukuru shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC) kwa kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuwahudumia watu wanaoishi na maambukizi ya VVU.
“Juhudi za mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi zitafanikiwa zaidi pia kama tutaboresha kamati za Ukimwi za ngazi ya kijiji na kata kwa ajili ya kubadilishana mawazo na uzoefu ili kupunguza maambukizi ya VVU katika mkoa wetu ambao maambukizi yameongezeka kutoka asilimia 4.2 hadi 7.2”,alisema Dk. Masele.
Naye Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona alisema lengo la mafunzo hayo ya msaada wa kisaikolojia ni kuwezesha upatikanaji wa huduma rafiki kwa watoto, vijana na watu wazima wanaoishi na VVU ili watambue umuhimu wao katika taifa na jamii zao.
“Mafunzo haya pia yatasaidia katika kutoa ushauri na mafunzo sahihi kwa watoto na vijana kuhusiana na majibu ya changamoto zinazowakabili, matumizi ya dawa/ARV na ufuasi mzuri wa dawa lakini pia kuboresha mawasiliano kati ya watoa huduma,wazazi, walezi, vijana na watoto”,aliongeza.
Aliyataja baadhi ya madhara yanayompata mtu iwapo atakosa msaada wa kisaikolojia kuwa ni pamoja na kukata tamaa ya maisha, kuacha dawa, kuchanganyikiwa, kujitenga ama kuwa na hali ya upweke na kupoteza maisha.
Shirika la AGPAHI linatekeleza miradi ya VVU na Ukimwi katika mikoa sita nchini ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Geita,Mwanza, Tanga na Mara likishirikiana na serikali ya Tanzania kupitia ufadhili wa serikali ya Watu wa Marekani kupitia CDC katika kutekeleza mradi wa “Boresha” ambao unatoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi mkoa wa Mwanza Dk. Pius Masele akifungua mafunzo kuhusu msaada wa huduma za kisaikolojia kwa wahudumu wa jamii. Kulia ni Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona.
Dk. Masele akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo watumie mafunzo wanayopewa ili wakaboreshe huduma kwenye vituo vya tiba na matunzo.
Dk. Masele akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia mbinu mbalimbali kurudisha wateja waliopotea.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada ukumbini.
Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona akielezea malengo ya mafunzo ya huduma na msaada wa kisaikolojia na maana yake kwa wahudumu wa jamii.
Cecilia Yona akielezea shughuli zinazofanywa na shirika la AGPAHI katika kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Gaston Kakungu ambaye ni Afisa Muuguzi Mstaafu akitoa mada wakati wa huduma na msaada wa kisaikolojia.
Kakungu akiwaasa washiriki wa mafunzo hayo kuwa daraja muhimu la kuunganisha wateja katika huduma za tiba na matunzo.
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Dk. Joseph Musagasa akielezea juu ya ukweli kuhusu VVU na Ukimwi.
Dk. Musagasa akiwasihi washiriki wa mafunzo hayo kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita imani potofu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi ya VVU, ikiwemo kuendekeza waganga wa kienyeji ambao baadhi yao hawana elimu ya kutosha kuhusu VVU na Ukimwi.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa