Benny Mwaipaja,
WFM, Mwanza
Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amekitaka Chuo Cha Mipango ya Maendeleo
Vijijini, kuhakikisha kuwa kinajielekeza kutatua changamoto zinazokwaza
maendeleo ya wananchi vijijini ili kuwafanya vijana wengi wanaokimbilia mijini
kutafuta maisha waweze kubaki kwenye vijiji vyao ambavyo vitakuwa vimepangwa
vizuri na kupatikana huduma muhimu za jamii
Dkt. Kijaji ametoa
rai hiyo mkoani Mwanza, baada ya kukagua maonesho ya bidhaa na huduma
zinazotolewa na chuo hicho katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa,
kilichoko eneo la Bwiru, mkoani humo.
Naibu waziri huyo
wa Fedha na Mipango amesema kuwa katika kufikia azma ya serikali ya kuwa nchi
ya viwanda ifikapo mwaka 2025, Chuo hicho kina wajibu mkubwa wa kufundisha wataalamu
watakao kuwa chachu ya kuboresha huduma na kuimarisha sekta ya kilimo ambacho
ndio nguzo kuu ya uchumi wa wananchi walio wengi vijijini.
“Ni muhimu
kuwafundisha kuwafundisha wakulima namna ya kuongeza thamani ya mazao yao,
badala ya kuuza vitunguu swaumu kilo moja shilingi 5,000, vikiongezwa thamani
tumeambiwa vitaunzwa kwa shilingi 24,000 kwa ujazo huo huo jamno ambalo ni
jema” aliongeza Dkt. Kijaji
Amesisitiza kuwa
Tanzania ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni ya viwanda ambavyo vimeanza
kuonekanana kuwataka watanzania kuwa tayari kuchukua fursa hizo, hususan vijana
mahali walipo kule vijijini badala ya kukimbilia mijini.
Kwa upande wake
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la
Ilemela, Jijini Mwanza, Bi. Angelina Mabula, amerejea wito wake kwa Halmashauri
zote nchini kutenga ardhi kwaajili ya kuendeleza vijana katika sekta ya
uzalishaji mali ili waweze kutumia uwepo wa Chuo cha Mipango katika
kuwaendeleza kwa vitendo kwa kuwapatia stadi za namna ya kujikwamua kiuchumi
Mkulima kutoka
Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, ambaye amewezeshwa na Chuo Cha Mipango kuongeza
thamani ya zao la Kitunguu Swaumu kupitia ufadhili wa Shirika la MIVARAF, Bw.
Boniface Bura, amempatia zawadi ya Kitunguu Swaumu kilichosindikwa, Rais Dkt.
John Pombe Magufuli, ikiwa ni ishara ya kuonesha furaha yake kwa mafanikio makubwa
aliyoyapata.
“Hivi sasa
ninauwezo wa kuvaa nguo mpya, nimepeleka watoto wangu shuleni na kujenga makazi
bora, hii ni fursa nzuri kwangu na wenzangu ambao kwa pamoja tumeamua kuongeza
mnyonyoro wa thamani wa zao letu la kitunguu swaumu” alisema Bw, Bura huku
akishangiliwa na watu walioshiriki kuangalia maonesho hayo
Naye Mkufunzi wa
Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Bw. Ezekiel Kanire, amesema kuwa Chuo
hicho kinafanya mawasiliano na Shirika la Viwango nchini TBS, ili iweze
kuwapatia wakulima hao wa Vitunguu wilayani Mbulu mkoani Manyara, namba ya
utambulisho ya ubora wa bidhaa ili bidhaa hizo ziweze kuuzwa pia kimataifa na
kuwaongezea wakulima hao kipato kikubwa zaidi.
Kupitia mpango huu
wa chuo wa kuwawezesha wakulima vijijini kupitia mradi wa Mivaraf, tumeweza
kuwasaidia wakulima wa vitunguu swaumu wa Mbulu mtambo wa kuchakata vitunguu
hivyo wenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 54, kinachobaki sasa ni
kuboresha zaidi uzalishaji na ufungashaji wa bidhaa hizo ili ziweze kupata namba
ya utambulisho kutoka TBS.
Bw. Kanire amesema
kuwa mpango huo utaanza mwezi Januari mwakani ambapo Chuo hicho kitakutana na
uongozi wa TBS ili kufanikisha jambo hilo litakalo kuwa mkombozi mkubwa kwa
wakulima ambao wataweza kupenyeza bidhaa zao katika soko la ndani na la
kimataifa.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment