Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence
Milanzi (wa kwanza kushoto), hii leo akizindua Jarida Maalumu la Taasisi ya
Taaluma za Wanyamapori Pasiansi (Pasiansi Wildlife Training Institute), iliyopo
Jijini Mwanza. Shughuli hiyo imeambatana na Uzinduzi wa Makala Maalumu ya
Miaka 50 ya taasisi hiyo.
Na BMG
Serikali imeahidi kuendelea
kuijengea uwezo Taasisi ya Taaluma za Wanyamapori iliyopo Pasiansi jijini
Mwanza, ili kukabiliana na matukio ya ujangili ambayo yametikisa nchi miaka ya
karibuni.
Akizungumza na wanahabari katika uzinduzi
wa Makala Maalumu ya Maadhimisho ya miaka 50 na Jarida Maalum la taasisi hiyo,
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi,
amesema taasisi hiyo imetoa mchango mkubwa katika kufundisha askari wanyamapori
ambao wamesaidia kwenye vita dhidi ya ujangili na kupunguza matukio ya ujangili
nchini.
Meja Jenerali Milanzi amesema katika
miaka ya karibuni Tanzania imetikiswa na matukio ya ujangili ambayo
yamesababisha kuuawa kwa wanyamapori wakiwemo tembo na kuhatarisha uwepo wa
wanyama hao ambao ni kivutio kikubwa cha watalii.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa
Taasisi ya Wanyamapori Pasiansi na vyuo vingine, serikali itaendelea kuvijengea
uwezo wa kifedha na rasilimali watu ili vitoe taaluma inayoendana na mahitaji
katika kukabiliana na matukio ya ujangili.
Mbali na
kuvijengea uwezo vyuo hivyo, Meja Jenerali Milanzi, amesema serikali pia
inatambua umuhimu wa wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo ya hifadhi na kwamba
itaendelea kuwaelimisha wananchi hao ili washiriki kikamilifu kwenye vita dhidi
ya ujangili.
Taasisi ya Taaluma za Wanyamapori Pasiansi (Pasiansi Wildlife
Training Institute) ilianzishwa mwaka 1966 hivyo kesho june 15,2016 inatarajia
kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
0 comments:
Post a Comment