Home » » SERIKALI KUKABILI UHABA WATUMISHI MAHAKAMANI

SERIKALI KUKABILI UHABA WATUMISHI MAHAKAMANI

KUTOKANA na uhaba wa watumishi katika mahakama nchini, Serikali inakusudia kutatua na kumaliza adha hiyo ambayo ni kero kwa wananchi.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro, kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa majaji Kanda ya Ziwa uliofanyika hoteli ya Malaika jijini hapa.
Dk. Migiro, alisema kumekuwepo na tatizo la ucheleweshaji wa kesi mahakamani kutokana na uhaba wa watumishi hususan waendesha mashitaka, kitendo ambacho kinawanyima haki wananchi.
Alisema kutokana na changamoto hizo, serikali imeamua kuongeza watumishi, waendesha mashitaka na mawakili ili kupambana na tatizo hilo ambalo linachangia kuwepo kwa migogoro ya muda mrefu.
"Serikali imeamua kuanza kufanyia kazi changamoto ambazo zilikuwa zikikabili mahakama zetu za Tanzania hususani wilayani na sasa tumeanza kuongeza watumishi na mawakili ili kuboresha sehemu zao za kazi," alisema na kuongeza.
"Tunaiomba jamii kutoa taarifa mahakamani endapo wataona kama kuna watumishi wa serikali ambao wanakiuka madili yao ya kazi kwa kuchukua rushwa," alisema Migiro.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman, alisema serikali imekusudia kupunguza miaka ya kuendesha kesi mahakamani, ambako kwa mahakama kuu inatakiwa kuendesha kesi kwa miaka miwili, mahakama ya mwanzo miezi sita na wilaya miezi 12.
Pia, alisema mfumo wa kutumia teknolojia ya zamani ya mawakili ama waendesha mashtaka kuandika katika vitabu kunasababisha kesi nyingi kuchelewa kusikilizwa, hivyo serikali inakusudia kuachana na utaratibu huo.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa