Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mvutano mkali umeibuka kati ya Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye
Viwanda na Kilimo (TCCIA) na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara
Mwanza (JMWM) kwenye kikao na Mkurugenzi wa jiji, Halfa Hida.
Mzozo huo uliibuka muda mfupi kabla ya kuanza
kikao cha ndani saa 4:00 jana asubuhi mjini hapa, kati ya
wafanyabiashara na mkurugenzi wa jiji, ambaye ilidaiwa aliwaalika TCCIA
bila kujua kama wanatofautiana kikatiba na jumuiya hiyo.
Katika kikao hicho, watumishi ya halmashauri hiyo
wakishirikiana na mgambo waliwazuia waandishi wa habari kuingia ukumbini
kwa madai kuwa hawakuwa wamealikwa.
Hata hivyo, muda mfupi wakati kikao hicho
kikiendelea, viongozi wa TCCIA wakiongozana na mwenyekiti wao, Eribariki
Mmari walitoka ukumbini wakidai kuwa wana dharura.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa
viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara waligoma kuendelea na kikao
wakipinga kuwapo kwa viongozi wa TCCIA, jambo lililosababisha mkurugenzi
wa jiji kuwaomba radhi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara,
Christopher Wambura aliwasilisha malalamiko yao kwa mkurugenzi, ikiwamo
kutozwa ushuru mkubwa tofauti na viwango vilivyowekwa.
Aidha, malalamiko mengine ni ongezeko la ushuru wa
taka, urasimu unaofanywa na ofisa masoko wa jiji na vitendo vya rushwa
vinavyofanywa na watoza ushuru.
Madai mengine ni mkurugenzi wa jiji kugoma
kukutana na wafanyabiashara hao wanapomhitaji. Mwananchi iliambiwa kuwa
Wambura aliomba viongozi wa TCCIA kutoka kabla ya kuanza kikao hicho
akieleza kuwa katiba ya jumuiya yao haiwatambui.
Hata hivyo, wakati kikao hicho kinaendelea, mgomo wa wafanyabiashara uliendelea kama kawaida na maduka mengi hayakufunguliwa.
Juzi, mwenyekiti wa TCCIA wa Mkoa wa Mwanza,
Elibariki Mmari alisema siyo sahihi kwa wafanyabiashara kugoma, kwani
tayari malalamiko yao yamewasilishwa kwa mkurugenzi wa jiji.
Pamoja na rai hiyo, jana maduka mengi yalikuwa
yamefungwa, huku polisi wakiwaonya baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa
wakiwazuia wenzao kufungua maduka kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria
na hatua kali zitachukuliwa kwa wote.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment