Home » » MWANZA YASIMAMA

MWANZA YASIMAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana,Ezekia Wenje.
 
Jiji la Mwanza limetikiswa na mgomo mkubwa wa umoja wa wafanyabiashara wakubwa na kati wa maduka ambao walifunga maduka kutwa nzima jana wakipinga kutozwa kodi kubwa. Hatua hiyo ambayo walidai ni ya kupinga maamuzi ya Jiji la Mwanza ya kuwatoza kodi kubwa katika biashara zao, ilileta usumbufu kwa wakazi wake kutokana na kukosa huduma muhimu.
Wakazi wengi waliotegemea kununua mahitaji yao ya vyakula katika maduka ya katikati ya jiji hilo hususani mitaa ya Libert, Rwagasore, barabara ya Posta, Lumumba, Kenyatta, Makoroboi na Nyerere, walihangaika na kujikuta hawana la kufanya.

Wafanyabiashara hao walishikilia msimamo wa kutofungua maduka yao wakidai wamechoka kuonewa na Halmashauri ya Jiji kwa kuwatoza kodi bila kuangalia vipato vyao halisi.

Wakizungumza na NIPASHE katika mitaa kadhaa, baadhi ya wakazi hao walisema mgomo huo ni chanzo cha ubabe wa viongozi wa Jiji kushindwa kukutana na umoja wa wafanyabiashara kuzungumzia matakwa yao.

WANANCHI WALALAMIKA
“Nimetoka Magu kufuata mahitaji muhimu madukani, lakini kila mtaa ninaokwenda nakuta maduka yote yamefungwa…nimetumia gharama kuja hapa na ninashindwa kuondoka nikiamini maduka yatafunguliwa,” alisema James Mabula, kutoka Magu.

Mabula alisema kitendo cha kufungwa kwa maduka hayo, kutamsababishia hali ngumu ya kimaisha kutokana na kutoondoka Mwanza hadi atakapofanikiwa kufunga mzigo wa kuondoka nao.

Mkazi mwingine, Diana Kimaro wa Soko Kuu, alisema serikali ndiyo imewasababishia matatizo ya kukosa kupata mahitaji yao muhimu kutokana na kufungwa maduka.

“Lazima serikali na hawa wafanyabiashara wakae pamoja kutatua kero hii…leo tunashindwa kununua mahitaji yetu kwa matakwa ya mtu mmoja ambaye hataki kukutana na wafanyabiashara,” alisema Kimaro.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mabatini, Yohana Mnumnu, alisema mgomo huo umeathiri wananchi wengi wakiwamo wale wanaotoka nje ya Jiji la Mwanza.

“Watu wamekuja kufuata bidhaa kutoka sehemu mbalimbali kama Sengerema, Magu na kwingineko, wanakuta maduka yamefungwa ni hasara kubwa kwao…huu ni ubabe wa Halmashauri ya Jiji kukaidi kukutana na wafanyabiashara,” alisema mwenyekiti huyo.

Mgomo huo pia umewaathiri wafanyabiashara wa vibanda vya mamalishe katika soko kuu la jijini hapa, waliosema wateja wao wakubwa ni wauzaji na wanunuzi katika maduka yaliyofungwa kwa ajili ya mgomo huo.

“Kwanza tumeshindwa kununua mchele kwa ajili ya kuwapikia wateja wetu, pia chakula tulichopika leo kimekosa wateja kutokana na kutokuwapo wanunuzi…tunaiomba serikali ikae na wafanyabiashara hawa kumalizia tatizo hili,” alisema Mama Madanganya mamalishe wa soko kuu.

Aidha, alisema kodi wanazotozwa na halmahauri ya jiji kila mwezi, ni kubwa na hivyo kuwa moja ya kero zinazolalamikiwa na wafanyabiashara hao. Baadhi ya wafanyabiashara walioamua kufunga maduka yao kwa ajili ya kuendesha mgomo huo kupinga ada kubwa za serikali wanazotozwa na jiji, manyanyaso ya askari wa Jiji, Mukeshi Vunjabei, alisema ili kuokoa tatizo hilo ni lazima mkurugenzi wa Jiji akae na kuafikiana nao.

“Manyanyaso ya kuchukuliwa mali zetu nje ya duka na zile za wateja, kulipa pesa nyingi za faini ni moja ya kero ambazo jiji linatufanyia wafanyabiashara,” alisema Vunjabei.

Vunjabei alisema wafanyabiashara wamekuwa wakinyanyasika sana na askari wa jiji pale bidhaa zao zinapowekwa nje ya duka kwa kuvutia wateja, nao huzichukua kwa kuvizia na kuondoka nazo.

Hata hivyo, mfanyabiashara mwingine, John Lema, alisema Halmashauri ya Jiji imekuwa na kero nyingi kwa wafanyabiashara hususani za kuwatoza ada mbalimbali zikiwamo za uchafu, leseni na kulazimishwa kulipia kifaa cha kuzimia moto (fire extinguisher).

“Hizi zote ni sehemu ambazo Jiji limekuwa likitukomoa kwa kututoza fedha, tunapewa malipo mengi yasiyo na maana, bidhaa zetu kunyang’anywa huku machinga wanaouza nje ya maduka yetu bila kulipa kosi wakiachwa,” alisema Lema.

MSIMAMO WA WAFANYABIASHARA
Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara hao, Christopher Wambura, alisema wataendelea na mgomo iwapo Jiji halitakubaliana na matakwa yao.

“Kesho (leo), tumeitwa na Mkurugenzi wa Jiji, lakini tunahitaji kuzungumza kuhusu madai yetu, na iwapo tukikubaliana maduka yatafunguliwa, lakini akigoma bado tutaendelea kufunga biashara zetu,” alisema Wambura.

WENJE AWAUNGA MKONO
Naye Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Ezekia Wenje, akizungumzia mgomo huo, alisema anawaunga mkono wafanyabiashara hao kutokana na serikali kushindwa wajibu wao wa kutowasikiliza.

Wenje alisema wafanyabiashara hao wana malalamiko ya msingi kutokana na sehemu wanazofanyia biashara kukumbana na changamoto mbalimbali zikiwamo za kuwapandishia kodi kutoka Sh. 12,000 hadi Sh. 300,000.

“Nawaunga mkono wafanyabiashara kwa mgomo huo, kwani serikali inajukumu la kukaa nao na kuwasikiliza…wasipofanya hivyo serikali inapoteza mapato kupitia mashine zake za EFD,” alisema Wenje.

KAULI YA MKURUGENZI WA JIJI
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Jiji, Halfa Hida, alisema mgomo huo hauna maana wala sababu zozote kwa kuwa madai yao yanazungumzika.“Nitakutana na viongozi wao kesho (leo), nitawasikiliza yale wanayoyahitaji, tukipata muafaka nitawaeleza wanahabari…lakini kwa sasa naona mgomo wao hauna maana,” alisema Hida.

Hida aliwataka wafanyabiashara hao kufungua maduka yao ili wananchi wapate mahitaji yao ya kila siku.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa