Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Benjamini Mkapa akizungumza wakati wa mkutano wa kujadili
Uwezeshwaji wa Afrika katika umiliki wa uchumi wake ambao uliandaliwa na
Taasisi ya Tanzania Professional Forum (Tanpro) na kufanyika Dar es
Salaam jana. Kulia ni Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Jaji Mstaafu, Raymond
Mwaikasu
Rais mstaafu, Benjamini Mkapa amempigia debe Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda kiana akisema ni kiongozi anayekubalika kwa wananchi,
hivyo wananchi wamuunge mkono kwenye nafasi yake ya sasa.
Pia, Mkapa amesema uadilifu wa Pinda ndiyo chanzo
cha watu kumwamini na kumkubali kutokana na kazi nzuri anayoifanya
serikalini, hivyo ni kiongozi mfano wa kuigwa.
Mkapa alitoa kauli hiyo juzi usiku wakati
akihitimisha harambee ya kuchangia fedha za mradi wa Mkapa Fellows kwa
ajili ya kusaidia kuboresha sekta ya afya vijijini iliyoendeshwa na
Pinda. Harambee hiyo iliandaliwa na Taasisi ya Benjamini William Mkapa
HIV/AIDS.
“Naomba niwaambie ndugu zangu, kiongozi mzuri ni
yule mwadilifu ambaye anakubalika kwa wananchi, hivyo naomba mumuunge
mkono Pinda katika kazi yake ya sasa. Nasema hivi kwa sababu wote
mmejionea wenyewe kazi aliyoifanya Waziri Mkuu hapa ni kubwa. Tumefanya
harambee na watu wameitikia kumuunga mkono, hivyo ni wazi kwamba
anakubalika na kuaminiwa na watu,” Mkapa alisema alipopewa nafasi ya
kutoa neno la shukrani katika hafla hiyo.
Kauli hiyo ya Mkapa imekuja siku moja baada ya
vyombo vya habari kumtaja Pinda kwamba ni miongoni mwa wanaCCM
wanaojipanga kuwania urais kupitia chama hicho.
Habari hizo zimedai kuwa tayari Pinda ameanza
kuzungumza na makundi mbalimbali kuhusu nia hiyo, wakiwamo wanaCCM
aliokutana nao mjini Mwanza juzi.
Kabla ya kuanza kwa harambee hiyo, Pinda alieleza jinsi alivyooteshwa kuwa harambee ingefanikiwa na ikawa hivyo.
“Sisi watoto wa Kifipa huwa tukioteshwa jambo
linakuwa la kweli na mimi usiku huu nilioteshwa kuwa harambee hii
itafanikiwa kwa kiasi kikubwa na kweli imefanikiwa,” alisema Pinda huku
akicheka.
Akizungumzia kuhusu uchangiaji fedha kwa ajili ya
mradi huo, Pinda alisema licha ya mafanikio makubwa kwenye sekta ya
afya, bado kuna changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni maambukizi ya Ukimwi
kitaifa kuwa asilimia tano, huku vifo vya kina mama wajawazito kitaifa
vikiwa juu kwa kina mama 454 kupoteza maisha kati ya wazazi 100,000.
Alisema Tanzania ina upungufu wa watumishi wa afya
kwa asilimia 52, jambo ambalo si la kuridhisha... “Katika Kanda hii (ya
Ziwa), asilimia 45 ya wanawake ndiyo wanaojifungua kwenye vituo vya
afya na wajawazito 500 hufariki kila mwaka, maambukizi ya Ukimwi ni
asilimia 4.8 na upungufu wa watumishi ni asilimia 39, hivyo kuna
changamoto kubwa inayotakiwa kufanyiwa kazi,” alisema Pinda.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Dk Ellen Senkoro
alisema Kanda ya Ziwa ni moja ya maeneo yaliyonufaika kupitia miradi ya
taasisi yake ikiwamo kuajiri watumishi mbalimbali wa kuhudumia miradi
yake.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment