Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Profesa Mwesiga Baregu, alisema inashangaza kwa Mkapa kukwepa kuzungumzia suala la mchakato wa katiba wakati inafahamika ni kiongozi mwenye msimamo.
Prof. Baregu ambaye alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema taarifa zilizopo ni kwamba ndani ya chama chake cha CCM, Mkapa alifanya ushawishi mkubwa kupendekeza muundo wa serikali mbili uwe ndiyo msimamo wa chama hicho na kupinga mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya serikali tatu.
“Mkapa ndiye mwasisi wa suala la uwazi, lakini sijui kwa nini uwazi unamshinda katika suala hili. Sijui alivyostaafu ndiyo uwazi nao ukaishia hapo,” alisema.
Alisema Mkapa kama kiongozi mkuu mstaafu wa nchi, anawajibika kuzungumzia suala la mchakato wa katiba hasa kutokana na hali tete iliyopo katika Bunge Maalum la Katiba kufuatia wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia Bunge Maalum la Katiba.
“Anakwepa kuzungumzia suala hilo mbele ya vyombo vya habari wakati ndani ya chama chake anakuwa wa kwanza kushawishi viongozi wenzake wakatae mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba... sijui kwa nini uwazi unamshinda katika suala hili,” alisema.
Prof. Baregu alidai vilevile kuwa Mkapa ndiye aliyeshawishi kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba awasilishe kwanza Rasimu ya Katiba bungeni kabla ya Rais Jakaya Kikwete kulizindua bunge hilo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana, alisema Mkapa na viongozi wengine wastaafu hawawezi kulikwepa suala la mchakato wa katiba mpya.
Dk. Bana alisema kwa kuwa Rais Mkapa ni mwanadiplomasia, inawezekana amesoma alama za nyakati na ndiyo maana anakwepa kuzungumzia suala la mchakato wa Katiba Mpya.
“Suala la mchakato wa katiba limekuzwa sana, hata watu wanaokwenda mahakamani kuhoji wamechelewa, walistahili kufanya hivyo mapema sana na siyo kusubiri hadi Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) wagome,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari, alisema kitendo alichokifanya Mkapa kujiweka kando na mchakato wa katiba ni cha busara kwa kuwa hataki kuonyesha mfungamano na upande wowote.
“Alichokifanya Mkapa ni cha busara kwani ameitunza heshima yake tofauti na viongozi wa serikali waliotoa misimamo hivi karibuni, mingi inaegemea ukiangalia inalenga kukwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya, alisema Prof. Bakari.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia (TGNP), Lilian Liundi, alisema kitendo cha Mkapa, kujiweka mbali kuzungumzia mchakato wa katiba ni cha busara.
“Ukiwa kiongozi ambaye uliwahi kuwa na madaraka makubwa unahitaji kufikiri mara mbili mbili kabla ya kuzungumza jambo ambalo linaigusa jamii kubwa, ,” alisema Liundi.
TUCTA: MKAPA YUPO SAHIHI
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Nicholaus Mgaya, amesena uamuzi wa Mkapa kutoingilia mchakato wa katiba mpya ni wa busara.
Alisema Mkapa ametumia busara na kuheshimu mchakato unaoendelea kwani kama angeongea angekwaza kundi moja wapo kati ya yanayotofautiana katika mchakato huo.
Alisema Rais huyo mstaafu ataendelea kuheshimika kutokana na ustaarabu na busara alizozitumia za kukaa kimya kuzungumzia suala hilo.
LHRC: MKAPA HAWATENDEI HAKI WATANZANIA
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema ukimya wa Mkapa kuhusiana mchakato wa Katiba mpya unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba hawatendei haki Watanzania.
Aidha, kimesema angetakiwa kutoa maelekezo pale anapoona mambo hayaendi vizuri kwa bunge hilo kwa kuwa amekuwa rais miaka kumi na anafahamu mambo mengi.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. Hellen-Kijo Bisimba, alisema busara za Mkapa zinahitajika katika kushauri juu ya mchakato huo na kutoa maelekezo bila kumuogopa kiongozi yeyote
“Mkapa akikaa kimya katika suala hili hawatendei haki Watanzania, busara za wazee kama yeye zinahitajika kwa kutoa ushauri bila kumuogopa kiongozi yeyote,” alisema.
Alisema akiendelea kukaa kimya watu watafikiri kuwa anaogopa kutoa ushauri kwa kuwa ataliudhi kundi la viongozi fulani wakati jamii inamwamini kwa kuwa kiongozi anayependa uwazi.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MUCCoBS), Dk. Tadey Msumanje, alisema hatua ya Mkapa kukaa kimya ni jambo la busara kwa kuwa wao ndiyo watakuwa wasemaji wa mwisho mambo kunasua mchakato utakapokwama.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji, alisema Mkapa kuzungumzia chochote kuhusu bunge hilo kungesaidia sana kunusuru mchakato huo.
Alisema viongozi kama hao wanapozungumza neno kuhusu taifa, huwa lina nguvu zaidi na kwa namna moja ama nyingine linaweza mawazo yao huchukuliwa kama ushauri.
“Rais Mkapa alikuwa katika nafasi nzuri ya kusaidia mchakato huu wa Katiba, hata angetegemewa hata kulitaka liahirishwe kwa sasa mpaka pale kutakapopatikana mwafaka wa kundi jingine ambalo limetoka katika bunge hilo,” alisema na kuongeza:
“Bunge hilo siyo sahihi kuendelea wakati wengine hawapo, japokuwa ni wachache, lakini kwa sababu ni vema na wao wakasikilizwa na viongozi wakuu kama hao ndiyo wanaweza kutoa ushauri wa kunusuru mambo makubwa kama hayo.”
WABUNGE WAZUNGUMZA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema kuwa ukimya huo wa Mkapa unaashiria kwamba anakwepa majukumu yake kama kiongozi wa mstaafu wa taifa anayeheshimika na mataifa mengi duniani kutokana na umahiri wake katika masuala ya kidiplomasia na usuluhishi.
Alisema huenda Mkapa msimamo wake ni ule ule ambao Kamati Kuu ya CCM imeutoa wiki iliyopita na kwamba ndiyo maana hataki kuzungumzia hilo kutokana na kuunga mkono msimamo wa chama chake.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema Mkapa kukaa kimya kuzungumzia mchakato wa katiba ni dalili ya kutokuwa na dhamira ya kutaka kusaidia kulikwamua taifa katika mgogoro ambao unatishia matumaini ya kupatikana kwa katiba yenye maridhiano.
“Mkwamo uliopo sasa unaweza ukaondolewa kwa busara ambazo zinatokana na uwapo wa marais wastaafu akiwamo Benjamin Mkapa ambaye bila shaka anaogopa kukemea na kushauri kama Watanzania wengine wanavyopendekeza kwa sababu tu ataonekana mbaya na chama chake,” alisema Selasini.
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la 201, ambaye hakutaka kutajwa jina lake litajwe, alisema Rais mstaafu amekataa kuzungumzia mwenendo wa bunge hilo kwa kuwa atachafuka kisiasa na kumshushia heshima yake mbele ya Watanzania.
Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM), Paul Makonda, alisema ni sahihi kwa Mkapa kukaa kimya kwa kuwa nia na matarajio ya Taifa yanajulikana lakini kwa hali ya kubezana.
Alisema heri akae kimya kwa kuwa ukimya nao ni jibu tosha.
TANGA WASEMA MKAPA YUPO SAHIHI
Kwa upande wa baadhi ya wananchi wa Jiji la Tanga walisema Mkapa kujiweka kando na mchakato wa Katiba mpya na Bunge Maalum la katiba ni uamuzi wa busara kwani mwenye mamlaka pekee juu ya suala hilo ni Rais Jakaya Kikwete.
“Mkapa ametumia busara kwa sababu sasa hivi kauli moja unayoitoa kila mtu anaitafsiri kivyake ukisema Bunge liendelee unaonekana wewe ni wa kundi hili ukisema livunjwe pia utaonekana ni wa kundi jingine,” alisema Onesmo Raymond.
Raymond ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Cambridge, alisema mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba umechangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha baadhi ya vyama vya siasa.
Naye Rose John Mwanaharakati wa masuala ya Maendeleo alisema huenda Mkapa alishatoa ushauri ambao haukufanyiwa kazi hivyo hana budi kukaa kimya na kuangalia Taifa linavyokwenda.
Omary Sekwao, alisema kuwa macho na masikio ya Watanzania kwa sasa yameelekezwa kwa Rais Kikwete ili kuhakikisha bunge hilo linaleta katiba iliyo bora na siyo bora katiba.
Jumamosi iliyopita wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya harambee ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa Hiv/Aids (BMAF), mradi wa Mkapa Fellows, jijini Mwanza, Mkapa alikataa kuzungumzia suala la mchakato wa Katiba.
“Sitaki kuzungumzia suala la Katiba Mpya wala mchakato wake unavyoenda,” alisema kwa kifupi Mkapa.
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Christina Mwakangale, Mary Geofrey, Jimmy Mfuru, Kamili Mmbando, Husein Ndubikile, Elizabeth Zaya Dar; Lulu George, Tanga na Godfrey Mushi na Salome Kitomari, Dodoma.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment