Tone

Tone
Home » » Sumaye atoa angalizo kuhusu elimu

Sumaye atoa angalizo kuhusu elimu

Waziri Mkuu mstaafu,Frederick Sumaye.
 
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema Tanzania inahitaji kuepuka uboreshaji elimu unaolenga kujitafutia sifa, wakati sekta hiyo ikikabiliwa na uduni wa viwango katika uhalisia wake.
Sumaye aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha mada kuhusu ‘maendeleo ya vijana na tatizo la ajira’, kwenye mkutano wa wanafunzi wa Chuo cha Biashara (Cobesa) cha jijini Mwanza uliofanyika jana.

Alisema uelimishaji wa wananchi hasa vijana wanaokua ni la msingi katika kujenga uchumi utakaomudu ushindani katika nyanja za sayansi na teknolojia na biashara za kimataifa.

“Tukiamua kuwekeza katika elimu bora badala ya bora elimu, tuhakikishe tunatoa elimu ya viwango vinavyokubalika na siyo elimu ya kujitafutia sifa isiyo na viwango,” alisema.

Alisema lazima elimu ijielekeze kwenye mahitaji halisi ya soko la wakati uliopo na la baadaye, inayomfanya mhitimu kuwa na taaluma katika ngazi aliyonayo hivyo kujiamini katika kazi.

Alivitaja viashiria vingine kuwa ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei na gharama za maisha, ukuaji wa uchumi wa taifa ulio endelevu na uwiano mzuri wa biashara kati ya bidhaa za ndani na nje ya nchi.

Sumaye, alizungumzia pia uchumi imara katika  ngazi ya familia na mtu mmoja mmoja, kwamba unategemea matunda ya uchumi mkubwa kumfikia kila anayefanya kazi.

Alisema, sehemu hii ya uchumi isiposimamiwa vizuri, watu wengi watabaki kuwa masikini huku uchumi mkubwa wa nchi ukikua na utajiri kubaki mikononi mwa wachache.

 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa