Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KATA ya Igogo imepata mafanikio makubwa ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Hayo yamebainishwa jijini Mwanza kwa nyakati tofauti na Diwani wa Kata hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Minja na Mwenyekiti wa CCM wa Kata, Michael Maungo katika mahojiano maalum na gazeti hili ambayo ndiyo yamezaa makala haya.
Kata ya Igogo ni miongoni mwa kata 12 zilizo katika wilaya ya Nyamagana yenye jumla ya wakazi 27,303, wanawake wakiwa 13,929 na wanaume 13,374 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Ni kata ambayo sehemu ya makazi yake ni ya milimani, eneo lingine likiwa kando ya Ziwa Victoria na wakazi wake wanajihusisha na shughuli za kilimo, viwandani na ujasiriamali. Utekelezaji wa miradi ya maendeleo Diwani wa Igogo, John Minja anasema katika kipindi cha mwaka uliopita utekelezaji wa ilani hiyo umewezesha wananchi wake kuwa na uhakika wa kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Minja anasema katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba mwaka jana, jumla ya miradi 20 iliyogharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 1.8 imetekelezwa katika kata yake. Miradi iliyokamilika ni ya ujenzi wa barabara ya Malalo iendayo katika taasisi ambapo ujenzi wa mitaro na kuiwekea moramu katika barabara hiyo uligharimu kiasi cha Shilingi milioni 66.
Miradi mingine kwa mujibu wake, ni ujenzi wa vyoo katika Shule ya Sekondari Igogo uliogharimu kiasi cha Sh 9,750,840 na ukamilishaji wa ofisi ya Mwalimu Mkuu Malulu uliogharimu kiasi cha Sh 8,033,160 na uwekaji umeme kwa Ofisi ya Mtendaji Kata kwa Sh 5,400,000.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa barabara ya lami ya Igogo –Pepsi iliyogharimu kiasi cha Sh bilioni 1.1 na ujenzi wa daraja la polisi Igogo uliogharimu Sh 8,660,000. Anasema mradi mwingine ni ujenzi wa maboma ya vyoo yenye jumla ya matundu 12 yaliyogharimu kiasi cha Sh milioni 10 na ujenzi wa vyumba sita vya madarasa katika sekondari ya Igogo uliogharimu kiasi cha Sh milioni 96.
“Tumekamilisha ujenzi wa choo cha Soko la Igogo kwa kushirikiana na Tasaf na nguvu za wananchi ambapo Tasaf imeweza kuchangia kiasi cha Sh 23,860,000,” anasema. Miradi mingine anasema ni wa umeme wa jua na maji katika Sekondari ya Igogo na ujenzi wa matundu 12 kwa ufadhili wa Tasaf iliyotoa Sh milioni 60.
Lingine lililofanyika anasema ni ujenzi wa maabara na kivuko cha watembea kwa miguu katika mtaa wa Igogo Kusini A kwa ajili ya Shule ya Msingi Azimio. “Tumeweka umeme kwenye ofisi ya kata na mtaa, tumekamilisha ujenzi wa ofisi ya Mwalimu Mkuu na darasa moja la Shule ya Malulu,” anafafanua.
Miradi mingine iliyotekelezwa ni ujenzi wa bwawa la samaki katani, ujenzi wa barabara ya Mansoor iendayo katika taasisi za umma na uwekaji wa mfumo wa majitaka katika mtaa wa Igogo Kusini A na Kaskazini B ambao unatumika hadi sasa. “Upembuzi yakinifu kwa ajili ya mitaa iliyosalia ya uwekaji mfumo wa majitaka umekamilika na ujenzi unatarajia kuanza mara moja na tumezindua kampeni ya usafi wa mazingira kwa mitaa yote ya kata,” anasema.
Minja ambaye pia ni Naibu Meya wa Jiji la Mwanza anaitaja miradi iliyokamilika kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Pepsi-Voil kwa kiwango cha lami na ule wa mtaro unaendelea sasa. “Tunatarajia kuanza ujenzi wa barabara ya mawe kuanzia ofisi ya CCM Kata hadi kwenye daraja liendalo katika ofisi ya kata,” anasema na kuongeza kwamba kata yake imeanzisha pia vikundi vya kusimamia sheria ya usafi wa mazingira.
Kwa upande wa mazingira anakiri hali sio nzuri, kutokana na jiografia ya kata, sehemu yake kubwa ni ya milima hali inayowawiwa vigumu kufanya usafi.
“Utunzaji na utupaji wa taka ni mgumu, watu wanatupa taka ovyo na unakuta taka katika kaya, biashara na kwenye taasisi, ingawa juhudi za kuhifadhi na kutunza mazingira zinaendelea licha ya wanaokusanya taka kutokuwa na uwezo wala vifaa vya kutosha vya kuzolea taka,” anaeleza.
Kwa upande wa kilimo na mifugo, anasema lipo tatizo la kuzagaa kwa mifugo hasa mbuzi na mbwa katika kila mtaa na kusababisha usumbufu. Kuhusu utawala bora, anasema kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na serikali za mitaa kwa kuunda kada ya maofisa watendaji wa mitaa, baadhi ya wenyeviti wa mitaa bado hawayaafiki mabadiliko hayo.
Katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, anasema kila mtaa unavyo vikundi vya kukopeshana vinavyotunza fedha kwa kuweka na kukopa kutoka taasisi za kifedha. Katika kuhifadhi mazingira, anasema kila kaya imeagizwa kupanda miti wa kuzunguka eneo lake ambapo taasisi zimeagizwa kupanda kiasi cha miti 250,000 ya aina mbalimbali.
Juhudi zinafanywa kupambana na rushwa na Ukimwi. Anasema rushwa na Ukimwi zimefanywa kuwa ajenda za kudumu kwenye vikao kuanzia ngazi ya mtaa hadi kata. Anasema kata yake inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za upungufu wa samani, madawati na majengo katika shule zilizo katika kata yake.
Changamoto nyingine ni ya kukithiri kwa utoro wa wanafunzi, ambapo katika kipindi hicho jumla ya wanafunzi 60 hawakuweza kuhudhuria masomo. “Walimu watano wameenda masomoni na kata ina jumla ya upungufu wa walimu 38, 20 ni wanawake na 18 ni wanaume. Tumepeleka maombi halmaashauri ione uwezekano wa kupata walimu waajiriwa wapya,” anafafanua.
Anasema kwa miradi tarajiwa iliyoanza mwezi julai 2013/14 ni pamoja na ujenzi wa kidato cha tano na sita, na kuongeza kuwa michoro ya ramani za majengo hayo imekamilika pamoja na makisio ya mradi. “Tunatarajia kukamilisha ujenzi wa madarasa sita ya Shule ya Sekondari Igogo na jengo la utawala, ukarabati wa matundu matatu ya choo katika Shule ya Msingi Igogo ujenzi wote unaendelea hivi sasa,” anaeleza.
Miradi mingine ni ujenzi wa Soko kuu la Igogo kwa ufadhili wa Mradi wa LVEMP unaotarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi milioni 437 na ujenzi wa wodi ya akinamama wajawazito katika Zahanati ya Igogo, ukamilishaji wa barabara zote za mitaa ambazo zimeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha gharama yake kamili inafanyiwa tathimini.
Utekelezaji wa kazi za Chama Mwenyekiti wa CCM Kata, Michael Maungo anasema safu ya uongozi wa chama katika kata umekamilika na unatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya chama. Uongozi huo unahusisha Kamati ya Siasa ya Kata, Madiwani wote wa CCM, viongozi wa jumuiya za chama, Kamati ya usalama ya maadili na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya kata.
Kuhusu uhai wa chama, Maungo anasema katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2013, chama hicho tawala katika kata kiliweza kuwapata wanachama wapya 326 na kufanya kata hiyo kuwa na jumla ya wanachama 2,408. Anakiri hali ya ulipaji wa ada katika chama bado sio wa kuridhisha, lakini anasema katika kipindi hicho, kati ya wanachama 2,408 ni wanachama 393 waliolipa ada.
“Chama tulipokea pendekezo la Halmashauri ya Jiji ya kuongeza mitaa mipya, ambapo tulipendekeza tuwe na mitaa mipya saba ili kufikisha jumla ya mitaa 13 na kata mpya moja,” anasema. Kwa upande wa vikao vya chama, Maungo anasema kata yake inaendelea kufanya vikao kwa mujibu wa Katiba ya CCM ingawa sio kwa asilimia 100.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment