Tone

Tone
Home » » Wachimbaji wadogo wa dhahabu kupata umeme

Wachimbaji wadogo wa dhahabu kupata umeme

WACHIMBAJI wadogo watapekewa umeme wa gridi ya taifa kwenye maeneo yote ya uchimbaji wa dhahabu kusaidia ajira na kuwapunguzia gharama ya kutumia jenereta na mafuta kwa mitambo yao ya kusaga na kuchenjulia dhahabu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele ambaye yupo na Rais Jakaya Kikwete kwenye ziara ya siku tano Mkoa wa Geita alikuwa akizugumza na wananchi wa Katolo na Busereserejana.

Alisema kutokana na kuwapo maeneo mengi ya wachimbaji wadogo amemuagiza Meneja wa Kanda wa Tanesco kuhakikisha umeme unafikishwa kwenye maeneo yote wanapochimba.

Agizo hilo alilitoa baada ya Mbunge wa Jimbo la Busanda, Lolencia Bukwimba kueleza kero za wananchi mbele ya Rais Kikwete.

Mbunge huyo lizitaja kuwa ni maji, barabara na kasi ndogo ya usambazwaji wa umeme.

Akizungumza na wananchi hao, Rais Kikwete alisema serikali yake itaendelea kutekeleza ahadi maeneo mbalimbali kwenye sekta zote kama alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2005 na 2010.

Wakati huohuo, Rais Kikwete alikunwa na uamuzi wa mwekezaji mzalendo kwenye sekta ya madini kwa kujenga shule ya msingi ya kisasa yenye ubora na hadhi ya sekondari na kuikabidhi kwa wananchi wa Kijiji cha Ng’azo wilayani Bukombe.

Mwekezaji huyo mzalendo, Emmanuel Gungu ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Nsagali Ltd. ya mjini Bariadi na amejenga vyumba vya madarasa saba, nyumba za walimu saba, jengo moja kubwa la utawala na kuweka samani za ofisi, maktaba moja ya kisasa, matundu manne ya vyoo vya walimu na matundu 21 ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi.

Akisoma taarifa mbele ya Rais Kikwete kwenye hafla ya kuzindua shule hiyo, Diwani wa Kata ya Ng’anzo, Thomas Masuga alisema mwekezaji huyo amekuwa mdau muhimu kusaidia jamii kwa kuchangia Sh 35,830,000 kwenye shughuli za maendeleo katika sekta za afya, elimu, barabara, maji na ujenzi.

Chanzo;Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa