MAHAKAMA ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, imemwamuru kwenda
gerezani siku 14 Mbunge wa Ukerewe, Salvatori Machemli (CHADEMA), kwa
kosa la kudharau mahakama.
Machemli ambaye anakabiliwa na kesi ya uchochezi, aliamriwa kwenda
gerezani jana baada ya kushindwa kuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi
yake.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima kutoka mahakamani hapo, zilisema
kuwa katika kesi hiyo, Machemli anadaiwa kutumia maneno ya uchochezi
katika mikutano mbalimbali ya hadhara wilayani humo mwaka jana, na
kwamba amekuwa akienda nje ya wilaya hiyo na hata nje ya nchi bila
idhini ya mahakama.
Inadaiwa kwamba, Machemli alipofika mahakamani hapo jana kwa lengo la
kuhudhuria kesi yake hiyo, alifutiwa dhamana kisha kuamriwa kuwekwa
ndani.
“Ni kweli mahakama imetoa amri ya kuwekwa ndani mheshimiwa Machemli
kwa kosa la kudharau mahakama. Alikuwa hahudhurii tarehe za kesi yake,
kutokana na hali hiyo, leo alipokuja mahakamani kuhudhuria kesi yake
aliondolewa dhamana kisha akaswekwa ndani,” kilisema chanzo chetu.
Ilidaiwa kwamba, hakimu anayesikiliza kesi hiyo alimtaka Machemli
kuwasilisha wadhamini wawili wapya wanaomiliki hati ya nyumba, ambao
walipatikana, lakini hakimu akabaki na uamuzi wake wa kutaka mbunge
huyo aende gerezani kwa siku hizo 14.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu, Machemli alithibitisha
kuondolewa dhamana kisha kuwekwa ndani kwa kosa la kudharau mahakama.
“Ni kweli wameniweka ndani. Ninapozungumza na wewe hapa nipo
mahakamani nasubiri wanipeleke ndani…daah haya ni majanga! Nilikuwa
nahudhuria vikao vya Bunge huku mahakamani sikuweza kufika.
“Lakini nilikuwa natuma watu wawili kuniombea ruhusa, sasa yawezekana
pengine hawakuwa wanakwenda ndiyo maana nimewekwa ndani,” alisema
Machemli.
CHANZO;TANZANIA DAIMA
|
0 comments:
Post a Comment