Home » » KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI AFANYA ZIARA YA KIKAZI MAGEREZA MKOANI MWANZA

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI AFANYA ZIARA YA KIKAZI MAGEREZA MKOANI MWANZA



 Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(Kaunda suti nyeusi) akimtambulisha Mhe. Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe kwa Wakuu wa Magereza Mkoa wa Shinyanga na Mkoa wa Mara baada ya kuwasili mapema asubuhi  katika Uwanja wa ndege wa Mwanza tayari kwa Ziara ya Kikazi katika Magereza Mkoani Mwanza leo

 Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(aliyepo kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Eng. Evarist Ndikilo( aliyepo kulia) mapema leo Julai 23, 2013 alipofika ofisini kwake kuweka sahihi katika Kitabu cha Wageni(mwenye shati jeupe) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(suti nyeusi) akiangalia Mashine Maalum ya kupimia Magonjwa mbalimbali wakati alipomtembelea Zahanati ya Gereza Butimba mapema leo Julai 23, 2013, anayeelezea ni Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Mariam Lumuli ambaye ni Mtaalam wa Maabara wa Zahanati hiyo. 
Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza

Na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza, Mwanza 
 Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amewataka Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Nchini kuzingatia Taratibu za kazi za kila siku katika Uendeshaji wa Magereza(Prisons Routine). 
 Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja ameyasema hayo leo wakati wa Ziara yake ya Kikazi katika Magereza Mkoani Mwanza alipokuwa akiongea katika Baraza la Makamanda na Askari wa Ofisi ya Magereza Mkoani Mwanza na Gereza Butimba, Mwanza. 
 Pia Kamishna Jenerali Minja ameongeza kuwa Makamanda na Askari watakao tenda kazi zao kwa ufanisi unaopimika watapandishwa vyeo ili kuwaongezea molari zaidi ya kazi ambapo amewataka wajitahidi zaidi kutenda kazi zao kwa weledi katika maeneo yao ya kazi. 
 Aidha amewatadhalisha Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza Nchini kuacha mara moja tabia ya kutumia nguvu kazi ya Wafungwa katika shughuli binafsi kinyume na taratibu za Uendeshaji wa Jeshi la Magereza. 
 "Tutaendelea kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa Maafisa na Askari watakaothibitika kutumia vibaya nguvu kazi ya Wafungwa kwa maslahi yao binafsi". Alisisitiza Kamanda Minja. 
 Kamishna Jenerali Minja pia amezungumzia mafanikio mbalimbali yaliyofanyika ndani ya Jeshi la Magereza tangu ateuliwe na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza.
Ametaja mafanikio hayo katika Jeshi ni pamoja na kukamilika kwa Karakana ya kutengeneza Magari katika Gereza Kuu Ukonga, Usajili wa Namba mpya za Magari ya Jeshi la Magereza, Kuanzishwa kwa Huduma za Maduka yanayouza bidhaa zisizo na Tozo la Kodi(Duty Free Shops) katika Mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma pia ujenzi unaendelea katika Mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro. 
 Mafanikio mengine ni pamoja na kukamilika kwa Jengo la gorofa kwa ajili ya makazi ya askari wa Magereza Mkoani Iringa, upanuzi wa Zoezi la Usafirishaji wa Mahabusu kutoka gerezani kwenda Mahakamani katika Mikoa ya Pwani, Arusha na Mkoa wa Dodoma ambapo zoezi linaendelea vizuri bila matatizo yeyote. 
 Kwa upande wao Maafisa na Askari wa Mkoa wa Mwanza wamempongeza Kamishna Jenerali kufanya Ziara yake Mkoani Mwanza ili kuweza kujionea changamoto mbalimbali zinazowakabili pamoja na kusikiliza shida mbalimbali za Maafisa na Askari. 
 "Tunampongeza sana Kamishna Jenerali Minja kwa uamuzi wake wa kuja hapa Magereza Mkoani Mwanza hasa kuja kuzungumza na sisi Askari wa Magereza Mkoa wa Mwanza tunaimani kubwa shida zetu zitapatiwa ufumbuzi kwa wakati kama ilivyokatika Utendaji wake wa kazi kuwa wa kasi na viwango". Alisikika Askari Mmoja wa Gereza Butimba, Mwanza. 
 Hii ni mara ya kwanza kwa Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja kufanya Ziara yake ya kikazi tangu ateuliwe rasmi tarehe 25 Septemba, 2012 kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa