MKUU wa Wilaya (DC) ya
Mwanza, Amina Masenza amewataka wajasiriamali 10 wa Kanda ya Ziwa waliopatiwa
vitendea kazi katika programu ya Safari Wezeshwa kuvitumia vema, ili viweze
kuwaendeleza kiuchumi.
Akizungumza na
wajasiriamali hao na wakazi wa jiji la Mwanza waliojitokeza kushuhudia tukio
hilo juzi katika Uwanja wa Furahisha, Masenza alisema ni wakati muafaka kwa
wajasiriamali hao kuinua maisha yao na jamii inayowazunguka.
“Kaweni mfano na
mabalozi katika jamii kupitia ruzuku hizi, waonyesheni TBL kuwa kuanzisha
programu hii hawajakosea bali ni ubunifu wa hali ya juu ambao utaleta tija na
baada ya muda jamii itatambua mchango wao kupitia haya wanayoyafanya sasa,”
alisema mkuu huyo wa wilaya.
Pamoja na hayo,
aliwataka waliokosa nafasi ya kupewa ruzuku wasikate tamaa, na kwamba wajaribu
awamu ijayo na kwa wale ambao hawajawahi kuomba wafanye hivyo.
Meneja wa bia ya
Safari Lager, Oscar Shelukindo, aliwataka wajasiriamali kuitumia vema semina
waliyopewa ya namna ya kuendesha biashara zao huku akiwahimiza kutumia vema
ruzuku hizo.
Shelukindo alisema
yuko tayari kumsaidia mjasiriamali aliyepiga hatua kwa kumuongezea kitu
alichokwama ili apige hatua zaidi ya maendeleo.
Programu ya Safari Lager
Wezeshwa ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ilianza mwaka juzi na hii ni mara ya
pili kutoa ruzuku kwa wajasiriamali.
CHANZO : TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment