Home » » Nyanza kununua kilo milioni tano za pamba

Nyanza kununua kilo milioni tano za pamba

CHAMA cha Ushirika mkoani Mwanza cha Nyanza Cooperative Union (NCU) kinakusudia kununua kilo milioni tano za pamba katika msimu wa mwaka 2013/2014 unaotarajiwa kuanza Julai, 2013. Kaimu Meneja Mkuu wa NCU, John Masalu, ameiambia MTANZANIA kuwa chama kimekamilisha taratibu zote za maandalizi kwa kuanza ununuzi mara tu baada ya msimu kuzinduliwa rasmi.
Alisema wanachama wa NCU kupitia vyama vyao vya msingi, wanapaswa kuuza pamba kwa chama chao cha ushirika na wamejipanga kuhakikisha wakulima wa zao la pamba mkoani Mwanza wananufaika.

Alisema chama hicho kinatarajia kutoa bei nzuri kwa wanachama pamoja na wakulima wa zao la pamba na kuwataka kujiepusha kuuza pamba yao kwa kampuni nyingine kwa utaratibu wa mali kauli.

“Wakati wa msimu wa pamba kuna baadhi ya wanunuzi ambao si waaminifu ambao wamekuwa wakiwarubuni wakulima na kuchukua pamba yao kwa mali kauli, hivyo wanapaswa kuwa makini wasiweze kurubuniwa,” alisema Masalu.

Kuhusu mtikisiko wa uchumi uliovikumba vyama vingi vya ushirika nchini, alisema madeni kutoka taasisi za fedha yenye riba kubwa yalichangia kuvivuruga vyama hivyo.

Aidha, aliipongeza Serikali kutokana na kuingilia kati na kulipa baadhi ya madeni vilivyokuwa vikidaiwa vyama vya ushirika hapa nchini.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa