na Sitta Tumma, Mwanza
CHAMA
cha Alliance for Demokratic Change (ADC), kimewalipua Rais Jakaya Kikwete na
mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, kwa madai kwamba wamehodhi rasilimali nyingi
za taifa kwa maslahi yao binafsi na familia zao, kinyume cha taratibu na sheria
za nchi.
Katika
utawala wake, Mkapa aliweza kujimilikisha shamba kubwa la miwa la Mtibwa huko
Morogoro pamoja na mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, huku Rais Kikwete
akituhumiwa kuhodhi rasilimali za madini.
Akihutubia
mkutano wa hadhara katika viwanja vya Igoma jijini Mwanza juzi, Katibu Mkuu wa
ADC, Lucas Limbu, alisema umaskini uliokithiri nchini unatokana na watawala
kujali maslahi yao binafsi badala ya taifa.
Alisema
kuwa kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kufumua mikataba ya kifisadi katika
sekta ya madini ni kielelezo tosha kwamba na yeye ana maslahi katika mikataba
hiyo.
“Watanzania
tunalalamika mikataba ya madini ni mibovu. Lakini Rais Kikwete amekaa kimya.
Hawa watu wamejipanga kunyonya rasilimali za taifa. Mkapa akiwa madarakani
aliingiza marafiki zake Ikulu ili wanyonye nchi. Alijimilikisha mgodi wa Kiwira
na shamba kubwa la miwa la Mtibwa. Kwa hiyo ADC inawaomba Watanzania waichukie
na wainyime kura CCM mwaka 2015,” alisema.
Katika
mkutano huo zaidi ya wanachama 200 walijiunga na chama hicho kwa kukabidhiwa
kadi mpya, huku kukiwa na upinzani mkali kutoka kwa wafuasi wa CHADEMA,
waliokuwa wakiitikia ‘Power’ kila ilipotamkwa salamu ya ADC kwa kunyoosha
vidole viwili vya alama ya ‘V’ juu.
Kwa
upande mwingine, Limbu alimshukia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akimtuhumu
kushindwa kusimamia vema majukumu yake na kwamba kwa sasa hawezi kumsimamisha
kazi mkuu wa wilaya wala mkoa.
Alisema
Pinda ni muoga wa kuchukuwa hatua, huku akitolea mfano sakata la aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, aliposhindwa
kumwajibisha bungeni baada ya kudaiwa kukusanya fedha kinyume na utaratibu.
Limbu
alifafanua kuwa ADC ikiingia madarakani itahakikisha inasimamia na kuboresha
zaidi sekta ya elimu na kuwa mradi wa kwanza wa serikali yake, kwani kwa sasa
sekta hiyo imetelekezwa wakiwemo walimu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment