na Jovither Kaijage, Ukerewe
BARAZA la Vijana la Wilaya ya ya Ukerewe, jijini Mwanza, limependekeza kuwepo kipengele cha sheria katika Katiba mpya ijayo cha kulinda vyombo vya habari ili kuviwezesha kutekeleza majukumu yake vema pasipo kuingiliwa na hata kufungiwa kama ilivyo sasa.
Pendekezo hilo limetolewa jana katika mdahalo wa siku moja ulioandaliwa na baraza hilo kwa ufadhili wa shilika la Forum Syd kupitia na kuchambua vifungu vya Katiba ya sasa kubaini sheria nzuri zinazotakiwa kubaki katika katiba ijayo.
Wakitoa maoni yao baadhi ya vijana walisema, baadhi ya sheria zilizopo katika katiba ya sasa ikiwemo sheria ya magazeti ya mwaka 1976, ni kikwazo kwa jamii ya Watanzania kupata habari zilizo sahii na kwa wakati.
Mmoja wa vijana hao, Msekwa Bita, alisema sheria hiyo inatumiwa kukandamiza vyombo vya habari na kuongeza kuwa, hivi karibuni sheria hiyo imetumika kulifungia gazeti la Mwanahalisi kwa madai ya uchochezi.
Katika maelezo yake zaidi ambayo yaliungwa mkono na washiliki wengi, alisema sheria hiyo mbali ya kutumika kuvifunga mdomo vyombo vya habari, pia ipo kinyume cha Katiba ambayo inataka kuwepo uhuru wa kutoa maoni na kupata habari.
Wakichangia maoni zaidi, pia vijana hao wametaka pia iwepo sheria ya kuwalinda wahandishi wa habari ambao mbali ya kujeruiwa na hata kuuawa, pia wanapewa vitisho, hali ambayo inayowafanya washindwe kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Naye mwezeshaji wa jamii na mlezi wa baraza hilo , Raphael Kulola mbali ya kuunga mkono maoni hayo, pia ametaka iwepo sheria ya kuwabana baadhi ya viongozi wanaokwepa kutoa habari pindi wanapotakiwa kufanya hivyo.
Katika hatua nyingine, vijana hao wametaka madaraka ya Rais yapunguzwe ikiwa ni pamoja na mawaziri wasitokane na wabunge ili kukiwezesha chombo hicho kutimiza wajibu wake vema wa kuisimamia serikali.
Akitoa maoni yake juu ya suala hilo, Catheline Athanas alisema ni vema nafasi za uwaziri zikaombwa kama kazi nyingine na kwa kufuata taaluma ili kupata viongozi wanaweza kuwajibika vema na kuleta maendeleo ya haraka.
Alisema, mfumo uliopo sasa wa kuwapata viongozi hao na wasekta nyingine mbali ya kumpa madaraka makubwa rais pia unaweza kusababisha kuteuliwa viongozi wasio na uwezo pamoja na nafasi hizo kutolewa kwa upendeleo.
Mwezeshaji wa jamii, Raphael Kulola , akizungumza katika mdahalo huo uliofadhiliwa na Shirika la Forum Syd, amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya ikiwa ndiyo njia pekee ya kupata katiba yenye masilahi ya wengi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment