Home » » ASKOFU ATAHADHARISHA KUHUSU UDINI

ASKOFU ATAHADHARISHA KUHUSU UDINI

na Stella Ibengwe, Sengerema
WATANZANIA wametakiwa kuwa makini na baadhi ya watu wenye lengo la kutaka kuwagawa watanzania kwa misingi ya udini ili  kuweka maoni yao kwa masilahi binafsi  katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya uundwaji wa Katiba mpya.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Muhashamu Baba Askofu wa Jimbo Kuu la Geita, Damian Dalu, wakati wa ibada ya misa takatifu iliyokwenda sanjari na kuwapa  Kipaimara vijana 172 wa Kanisa Katoliki  Parokia ya Kristu Mfalume mjini Sengerema, mkoani Mwanza.
Askofu Dalu aliwataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa ujumla kushiriki kutoa maoni yao ili kupata Katiba iliyo bora na kuendelea kuwaombea viongozi na taifa zima wanaosimamia mchakato huo waweze kufanya kazi zao vizuri na hatimaye Katiba mpya iweze kupatikana.
Akizungumzia suala la migomo ya madaktari na walimu, alisema imesababisha mvutano mkubwa kati ya pande zote mbili serikali na watumishi hao  huku wanaoumia ni watu wanaokwenda kupata huduma za matibabu hospitali pamoja na wanafunzi wanaoshindwa kupata elimu ambayo ndiyo msingi wao wa baadaye.
“Mnapofanya migomo msitangulize mbele maslahi, daini kwanza kuboreshewa mazingira yenu ya kazi…..hivi wewe mwalimu unafundisha wanafunzi wamekaa chini, darasa halina hata sakafu, na vifaa vya kufundishia hakuna, unategemea huyu mwanafunzi atakuelewa? Mkifanya mgomo wa kutofundisha mpaka mboreshewe mazingira mtakuwa mmefanya jambo la maana.”
Aliongeza: “Mazingira yakiboreshwa hata hiyo mishahara yenu mnayodai itaboreshwa, vilevile kwa madaktari unadai kupandishiwa mshahara wakati hakuna vifaa, madawa, vitanda wagonjwa wanalala chini, japokuwa kwa madaktari katika madai yao suala la vifaa lilikuwepo lakini serikali nayo upande mwingine inatakiwa kulaumiwa kwa kuwa imeangalia upande wa mishahara tu, mengine yakaachwa.”
Askofu Dalu aliishauri serikali kuangalia madai hayo kwa umakini mkubwa kutokana na baadhi yake kuwa ni ya msingi badala ya kuchukua hatua, jambo ambalo linasababisha mvutano kati ya serikali na watumishi wake, jambo ambalo ni hatari.
Hata hivyo hakusita kuzunzungumzia suala la vitendo vya kikatili vinavyofanyika katika jamii yakiwemo mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na vikongwe kwa tamaa ya kujipatia utajiri wa haraka, na ameitaka jamii imrudie  Mungu kwa kuwa yeye ndiye muweza wa yote.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa