Home » » MBUNGE ADAI KUNA MELI IMEBADILISHWA JINA ZIWA VICTORIA

MBUNGE ADAI KUNA MELI IMEBADILISHWA JINA ZIWA VICTORIA

Na Maregesi Paul, Dodoma
MBUNGE wa Ole, Rajab Mbarouk (CUF), amesema kuna meli ya mizigo imebadilishwa na kuanza kusafirisha abiria katika Ziwa Victoria.

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali isipochukua tahadhari, meli hiyo inaweza kuzama na kusababisha vifo kama ilivyotokea katika Meli ya Mv Skagit, iliyozama hivi karibuni kisiwani Zanzibar.


Mbarouk alitoa taarifa hiyo bungeni jana, alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.


“Meli ya MV Skagit, ilizama kwa sababu baada ya kununuliwa na wafanyabiashara wa Zanzibar kutoka Marekani, ilibadilishwa muundo wake na ikaanza kubeba abiria.


“Kutokana na mabadiliko hayo, mwishowe meli hiyo imezama na kuua makumi ya wananchi kwa sababu hata ukifuatilia historia yake, inasemekana ilikuwa ikitakiwa kusafiri umbali usiozidi kilomita saba.


“Kwa hiyo, kama tahadhari isipochukuliwa, yaliyotokea Zanzibar yanaweza kutokea katika Ziwa Victoria, kwa sababu kule kuna meli inaitwa Sumar II inasafirisha abiria kutoka Mwanza kuelekea Nansio Ukerewe na wakati mwingine inakwenda Uganda.


“Meli hii, inayobeba abiria zaidi ya 200 ilikuwa ni ya mizigo, lakini sasa imebadilishwa matumizi yake, kwani inabeba abiria, iangalieni sana meli hii ili yasije yakatokea yaliyotokea Zanzibar,” alisema Mbarouk.


Awali wakichangia bajeti hiyo, baadhi ya wabunge waliishangaa Serikali ya Tanzania kwa kutokuwa na usafiri wa uhakika wa ndege.


Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema haridhishwi na utendaji kazi wa Serikali kwa kutokuwa na ndege wakati Rwanda ambayo ukubwa wake ni sawa na Mkoa wa Kigoma ina ndege saba.


Naye Mbunge wa Viti Maalum, Anamery Malaki (CHADEMA), alisema ni aibu nchi kama Tanzania kukosa ndege ya abiria wakati ina utajiri kuliko nchi nyingi duniani.


Wakati hao wakisema hayo, Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Pudenciana Kikwembe (CCM), naye alisema haiingii akilini kwa nchi kama Tanzania kukosa ndege wakati Ethiopia ina ndege nyingi.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa