Home » » MADIWANI CHADEMA WAMLIPUA WENJE

MADIWANI CHADEMA WAMLIPUA WENJE



Na John Maduhu, Mwanza
BAADHI ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamemlipua Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, kuwa alitoa lugha za vitisho kwa madiwani waliopiga kura ya kutokuwa na imani na aliyekuwa Meya wa Mwanza, Josephat Manyerere.

Wakizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, madiwani hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema walipigiwa simu usiku wa kuamkia siku ya kikao na Wenje, akiwaeleza watakiona cha moto endapo watakwenda kupiga kura ya kutokuwa na imani na Manyerere.

Madiwani hao wameeleza kauli hizo za vitisho hawakukubaliana nazo, kwa kuwa Manyerere tayari alikuwa ameshindwa kujibu tuhuma 11 zilizokuwa zikimkabili na alikuwa akipigiwa chapuo la kubaki madarakani na Wenje, kutokana na kuwa na maslahi binafsi katika uongozi wake.

Walisema walitakiwa kutokwenda katika kikao kilichoitishwa kwa ajili ya kumjadili Manyerere kutokana na hoja iliyokuwa imewasilishwa na madiwani 17 ya kutokuwa na imani naye.

“Kauli hizo za vitisho hakika ziliwakasirisha madiwani na kuapa kuingia katika kikao hicho na kupiga kura, Wenje alikuwa siku zote akimkingia kifua Meya, licha ya udhaifu wake wa kiuongozi kwa kuwa alikuwa na maslahi yake binafsi kwa kuwasaidia baadhi ya jamaa zake kupata zabuni,” alisema mmoja wa madiwani hao.

Madiwani hao walisema mbali ya Wenje, baadhi ya viongozi wa ngazi ya mkoa na Taifa walikuwa wakipiga simu kwa madiwani kuwatisha wasipige kura ya kutokuwa na imani na Manyerere.

“Chama chetu kina matatizo makubwa, kuna mgawanyiko mkubwa baina ya madiwani, kikubwa ni mgongano wa maslahi binafsi, viongozi wetu wa ngazi ya mkoa na Taifa nao wameingia katika makundi hayo, muda wowote Chadema inaweza kusambaratika endapo kazi ya ziada haitafanyika kuokoa matatizo yaliyopo,” alisema mmoja wa madiwani hao.

MTANZANIA lilimtafuta Wenje kuzungumzia malalamiko hayo ya madiwani, lakini hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita mfululizo bila kupokelewa.

Chanzo: Mtanzania


0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa