na Sitta Tumma, Magu
ASASI ya TCSD inayojishughulisha na uangalizi wa miradi inayotekelezwa na LVEMP II, imesema zaidi ya tani 40 za uchafu humwagwa kila mwaka katika bonde la Ziwa Victoria, jambo linalohatarisha maisha ya wananchi wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, zinazotegemea maji ya bonde hilo.
Kutokana na hali hiyo, imeelezwa zaidi ya watu milioni 150 wa ukanda wa nchi hizo wapo hatarini kuathiriwa na uchafu huo iwapo mikakati thabiti na endelevu haitachukuliwa kwa haraka.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Magu juzi na Mratibu wa Asasi ya TCSD, Dk. Sam Kasulwa, kwenye kikao cha robo mwaka cha wadau wa LVEMP kilichowashirikisha maofisa watendaji wa kata, vijiji na wenyeviti wa vijiji wilayani humo.
Alisema takwimu za kitaalamu zinaonesha upo ulazima wa jamii ya Wilaya ya Magu na Kanda ya Ziwa kushirikiana kupiga vita uchafuzi wa mazingira katika bonde hilo na kwamba kufanya hivyo ni kwenda sambamba na sera zilizoridhiwa kimataifa katika kutokomeza uchafuzi wa mazingira.
Kwa mujibu wa mratibu huyo wa TCSD, uchafuzi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya watu katika wilaya hiyo na kwingineko nchini ni chanzo kikuu kinachosababisha kupungua kwa hewa ya Oksijeni, hivyo kuharibu mazalia ya samaki na kusababisha rasilimali hiyo kupungua.
“Taarifa za kitaalamu zinaonesha kila mwaka zaidi ya tani 40 za uchafu humwagwa ndani ya bonde hili. Hii ni hatari kwa maisha ya watu wa nchi zinazotegemea maji ya bonde hili,” alisema.
Hata hivyo, Dk. Kisulwa aliwaomba viongozi wa serikali, taasisi, mashirika, makampuni na wananchi wa Wilaya ya Magu kushirikiana kutekeleza miradi hiyo, ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment