Na John Maduhu, Mwanza
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Kamati ya Madiwani ya chama hicho, kimetoa siku nne kwa Meya wa Halmashauri ya Mwanza, Josephat Manyerere, kuachia madaraka yake.
Madiwani wa chama hicho wameamua kumpa siku nne Manyerere ambaye pia ni mwanachama mwenzao kutokana na kushindwa kujibu kwa ukamilifu tuhuma 11 zilizowasilishwa kwake kutokana na kutorizishwa na uongozi wake tangu achaguliwe zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani zilizopatikana zimeeleza kuwa, Manyerere alipashwa kuwasilisha utetezi wake kwa maandishi juu ya tuhuma 11 zilizowasilishwa kwake na madiwani wa chama chake kabla ya Alhamisi ya wiki iliyopita.
Taarifa hizo zimeelezea kuwa baada ya kukabidhiwa tuhuma hizo, alishindwa kuzijibu ambapo kwa mujibu wa utetezi wake ameshindwa kuweka wazi na badala yake ametoa majibu ambayo yamezidi kujenga makundi.
“Madiwani kupitia kamati yetu pamoja na viongozi hatukukubaliana na majibu yaliyowasilishwa na Meya kutokana na tuhuma zinazomkabili, hivyo kwa kauli moja tumeamua kumpatia siku nne hadi Jumatatu awe ameachia ngazi mwenyewe vinginevyo tutampigia kura ya kutokuwa na imani naye katika kikao cha Baraza la Madiwani, kinachotarajiwa kufanyika wiki ijayo,” alisema mmoja wa madiwani wa viti maalumu wa Chadema.
Hata hivyo, Manyerere hakupatikana kuzungumzia sakata hilo kutokana na simu yake ya mkononi kuita mfululizo bila kupokelewa.
Hivi karibuni madiwani wa Chadema kupitia kamati yao walitoa tuhuma 11 dhidi ya Meya huyo na kumtaka kuzijibu kwa maandishi juu ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment