Na John Maduhu, Mwanza
MEYA wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere, amekalia kuti kavu baada ya madiwani wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwasilisha tuhuma lukuki dhidi yake na kumtaka kujipima mwenyewe na kuachia ngazi kabla ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.
Tuhuma hizo ziliwasilishwa na madiwani wa Chadema katika kikao cha kamati ya madiwani wa chama hicho kilichoketi juzi ambapo Manyerere amewasilishiwa tuhuma nzito 11 anazotakiwa kuzijibu hadi kufikia Alhamisi ya wiki hii na kuachia mwenyewe madaraka.
Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizoifikia MTANZANIA na kuthibitishwa na Manyerere ambaye naye ni diwani wa Chadema, zimeeleza kuwa madiwani hao wameamua kufikia uamuzi wa kuwasilisha tuhuma dhidi yake katika kikao cha chama kuhakikisha anaondoka madarakani.
Tuhuma alizosomewa katika kikao cha chama hicho kuwa ni kushindwa kuwaunganisha madiwani na kusababisha mpasuko na kuzalisha makundi kitendo ambacho madiwani hao wamekieleza kuwa ni hatari katika kujenga chama.
Tuhuma nyingine dhidi yake ni kushindwa kusimamia vikao vya Halmashauri ya Jiji hali inayosababisha vurugu na vikao hivyo kuvunjika bila kufikia mwafaka kila wakati anapokuwa mwenyekiti.
Tuhuma ya tatu dhidi yake ni kushiriki kusimamia ujenzi wa Kanisa la Waadiventista analo abudu bila kanisa hilo kuwa na vibali vya ujenzi na amekuwa akisimamia yeye binafsi ujenzi huo ambao ni kinyume cha utaratibu na kutokuwa na vibali vya ujenzi.
Aidha, anatuhumiwa kushinikiza madiwani kugomea bajeti ya mwaka huu kwa kuwasomea barua ya kuwashinikiza huku akijua kuwa ni yeye mwenyewe ndiye aliyekiitisha huku kikiwa na upungufu mkubwa.
Tuhuma ya tano ni kitendo chake cha kusimamia na kushinikiza kufanyika kwa malipo dhidi ya kampuni moja iliyopewa zabuni ya kufuga mamba lakini haikuwahi kufanya hivyo huku akijua kuwa kampuni hiyo haikuwa na mkabata rasmi na Halmashauri ya Mwanza.
Tuhuma ya sita aliyosomewa ni kuigeuza Ofisi ya Meya wa Jiji la Mwanza kama mahakama na kuingilia majukumu ya kamati nyingine kinyume cha kanuni na kuifanya ofisi ya Meya kuwa na msongamano wa wananchi siku zote.
Tuhuma ya saba dhidi ya Manyerere ni kutumia vibaya Mfuko wa Meya kwa kuimarisha kanisa lake kwa kulipatia fedha toka mfuko huo ambapo pia ameshindwa kuzitolea maelezo fedha hizo kwa mujibu wa kanuni za halmashauri.
Katika tuhuma ya tisa, anadaiwa kushindwa kujenga upendo na uhusiano na madiwani wenzake na kuwa mbinafsi kwa kushindwa kuwahudumia ambapo anadaiwa kuwashusha katika gari lake na madiwani na kuwapatia kiasi cha Sh 1,000 kwenda nyumbani kwao badala ya kupelekwa na gari la Meya ambalo limekuwa likihudumiwa na halmashauri kwa mafuta na matengenezo.
Tuhuma ya 10 dhidi ya Meya huyo ni kutumia cheo chake kwa upendeleo kwa kuwalazimisha wakuu wa idara kutoa upendeleo wa wazi katika kupeleka miradi mbalimbali katika kata yake huku kata zingine zikibaki bila kuwa na miradi.
Tuhuma ya 11 dhidi ya Meya huyo ni kusimamia uhamishaji wa miliki ya Shule ya Msingi Mbugani bila idhini ya vikao husika hali iliyosababisha usumbufu kwa wananchi na kuichonganisha halmashauri hiyo na wananchi.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu, Manyerere, alikiri kujadiliwa katika kikao cha chama hicho na kusomewa tuhuma dhidi yake na kutakiwa kujipima mwenyewe.
“Hapa nilipo niko naandaa majibu ya tuhuma hizo, nikimaliza kuzijibu tuhuma hizo nitaziwasilisha katika sehemu husika kwa ajili ya hatua zaidi hivyo sina cha kusema kwa sasa,” alisema Manyerere.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment