Home » » Mwenyekiti Halmashauri Misungwi kikaangoni

Mwenyekiti Halmashauri Misungwi kikaangoni


na Sitta Tumma, Mwanza
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mwanza, kimesisitiza kuwa msimamo wake wa kumtaka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Benald Polcarp kujivua 'gamba' ipo pale pale na kwamba tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazomkabili ni nzito.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina alipozungumza na Tanzania Daima, na kusema Polcarp ni lazima awajibike kwa kuachia nafasi yake hiyo aliyopewa na madiwani kwa dhamana ya chama.
Polcarp anadaiwa kutajwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa matumizi mabaya ya madaraka, ikiwa ni pamoja na kujipatia zabuni za ujenzi ndani ya halmashauri hiyo kupitia kampuni yake, kinyume cha sheria na taratibu za nchi.
Akifafanua kuhusu tuhuma hizo, Mabina alisema maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Misungwi kumtaka Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ajivue 'gamba' kutokana na tuhuma nzito zinazomkabili, hayana lelemama wala mjadala, bali lazima yatekelezwe kwa vitendo.
Kwa upande wake, Polcarp alipotakiwa kuzungumzia suala hilo aliushangaa uongozi wa chama chake kumng'ang'ania aachie nafasi yake, na kuhoji kwamba kama kweli tuhuma hizo ni za kweli kwa nini hajafikishwa mahakamani.
Alisema tuhuma anazohusishwa nazo hazifahamu kwani hajaiona ripoti ya CAG, na kwamba anachoamini ni kwamba kuna mkakati wa muda mrefu wa kummaliza kisiasa unaofanywa na baadhi ya watu wilayani humo, hivyo ni vema chama kikaacha kuingilia mambo kama hayo kwani yeye hana hatia yoyote.
“Mimi sijaiona hiyo ripoti ya CAG yenye tuhuma zangu. Lakini nashangaa chama kuning'ang'ania...maana huu ni mkakati unaofanywa ili kunimaliza kisiasa. Kwani wewe mwandishi umeiona hiyo ripoti unisaidie?” alihoji Polcarp huku akivilaumu vyombo vya habari kwa madai kwamba vinapotosha ukweli wa mambo.
Chanzo: Tanzania Daima


0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa