Na John Maduhu, Mwanza
HALI ya mambo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza si shwari, baada ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa kumtuhumu mwenyekiti wao, Clement Mabina, kuendesha chama kibabe.
Pia wajumbe hao, wamepinga uamuzi wa kumvua madaraka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi, Bernard Pollycap.
Wajumbe hao, Boniface Magembe na Sarah Ng'hwani, waliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana, kuwa wamesikitishwa na taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa kamati yao, imefikia uamuzi wa kumvua madaraka Pollycap.
Magembe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Mwanza, alisema kikao cha kamati ya siasa kilichoketi juzi, hakikufikia uwamuzi wowote.
Alisema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Mabina ambaye anadaiwa kuwa haelewani na Pollycap, alikuwa aking'ang'ania kuvuliwa uenyekiti Pollycap, lakini wajumbe wote walikataa, kwa vile kamati hiyo haina mamlaka kwa mujibu wa kanuni na katiba ya chama chao.
"Suala la tuhuma haliwezi kumuondoa mwenyekiti hadi pale vyombo vya dola vitakapothibitisha, Mabina anatuhumiwa kupora mashamba ya wananchi wa Kata ya Kisesa na suala hilo lilifikishwa katika vikao vya CCM na mkuu wa mkoa alimkingia kifua, alipaswa kuwajibika kwa kuachia madaraka," alisema Magembe.
Naye Sarah Ng'hwani, alisema anashangazwa na Kamati ya Siasa kulishwa maneno bila wao kujua.
Katibu wa Uenezi wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, Saimon Mangerepa, alisema yeye ni msemaji tu wa chama baada ya vikao kukaa na kufanya uamuzi.
Kwa upande wake, Majumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mwanza, Richard Rukambura, alisema wanasubiri suala hilo lifikishwe kwenye kikao cha Halmashauri ya Mkoa ili lijadiliwe kwa kina.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment