na Sitta Tumma, Mwanza
HATIMAYE Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mwanza, kimemvua nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani hapa, Bernald Polycarp, kutokana na tuhuma za ufisadi wa fedha za miradi ya maendeleo wilayani humo zinazomkabili.
Uamuzi huo ulitolewa juzi na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza, chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Clement Mabina, baada ya kile kinachodaiwa Polycarp kukaidi maagizo ya chama hicho kupitia kamati yake ya siasa iliyomtaka kiongozi huyo kujiuzulu nafasi hiyo.
Akitoa taarifa ya kikao cha kamati hiyo jijini hapa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM mkoani Mwanza, Simon Mayunga Mangelepa, alisema CCM imelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kiongozi huyo kukaidi maamuzi ya chama ngazi ya wilaya.
Mangelepa alieleza chama kinajiandaa kupeleka taarifa rasmi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, ili afanye utaratibu wa kuitisha uchaguzi mwingine wa kushika nafasi hiyo.
“Kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Mwanza, imemvua nafasi ya uenyekiti wa halmashauri ya Misungwi, Bernald Polycarp. Uamuzi huu umefikiwa baada ya kujiridhisha na tuhuma zilizoko kwenye ripoti ya CAG,” alisema Mangelepa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Clement Mabina, aliiambia Tanzania Daima jana ofisini kwake kwamba hatua ya Polycarp kuvuliwa nafasi ya uenyekiti wa halmashauri hiyo imerahisisha vyombo vya dola kufanya kazi zake vizuri juu ya tuhuma zinazomkabili kiongozi huyo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment