na Mwandishi wetu, Mwanza
KAMPUNI ya simu za mikononi ya Airtel imezindua mtambo wa mawasilano katika mkoa wa Kanda ya Ziwa nje kidogo ya mkoa wa Mwanza katika wilaya ya Misungwi ikiwa ni mkakati wake wa kufikisha huduma zake vijijini.
Akizindua mnara huo mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Nyamayinza, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga, alisema maendeleo vijijini yatakuwa kwa kasi iwapo wananchi watatumia mawasiliano ya simu za mikononi kutafuta masoko ya madini, mifugo au vyakula sehemu mbalimbali nchini.
“Mawasiliano yana faida kubwa duniani na ndio hufanya maendeleo ya jamii kwenda kwa kasi, hivyo wananchi wa vijiji vyote vinavyoizunguka Nyamayinza tumieni fursa ya kupata mawasiliano haya kwa kuendesha au kuendeleza biashara zenu.
“Anzisheni biashara za kutuma na kupokea pesa za Airtel Money na mtumie mawasiliano haya kutafuta wateja katika bidhaa za kilimo na mifugo mnazozalisha,” alisema.
Naye Meneja Mauzo wa Airtel Kanda ya Ziwa, Galus Mgawe, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, alisema kampuni hiyo imedhamiria kutoa mawasiliano ya uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kuzinduliwa kwa mtambo huo kutawezesha zaidi ya watu 15,000 walioko vijiji vya Nyamainza, Buhunda, Ishokela, na Seke kuwasiliana na ndugu na jamaa kwa uhakika.
Akizungumzia mpango wa kusambaza mtandao, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando, alisema, “Kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za mawasiliano kutokana na mazingira au kupanuka kwa shughuli za jamii husika ndiyo yanayotufanya Airtel kuitikia wito na kupanua zaidi wigo wa mtandao wetu kwa eneo husika.”
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment