Home » » CHUO CHA DENMARK CHAIPA MISUNGWI MISAADA

CHUO CHA DENMARK CHAIPA MISUNGWI MISAADA


na Sitta Tumma, Misungwi
CHUO cha Grenaa Free Production School cha nchini Denmark, kimetoa misaada ya vifaa mbalimbali zikiwemo kompyuta 90, vitanda vya hospitali 50, viti vya kubebea wagonjwa 20 na tanki moja la maziwa, wilayani Misungwi, Mwanza.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya sh milioni 200, vimetolewa juzi wilayani hapa kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu, kuboresha huduma za afya na miradi ya maendeleo wilayani Misungwi.
Mratibu wa Grenaa Free Production School hapa nchini, Jefta Kishosha, na msaidizi wake, Sebastian Maguta, walikabidhi vifaa hivyo kwa Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kishosha alisema komyuta hizo zimegawiwa katika shule za sekondari za Misungwi za Paul Boman, Misasi na Busongo, na kwamba kila shule imepatiwa kompyuta tano, huku Ofisi ya CCM Wilaya ya Misungwi nayo ikipatiwa kompyuta tano.
Kompyuta nyingine zimegawiwa Vituo vya Walimu (TRC), vya Kasololo, Mbarika, Usagara, Mwawile na taasisi za kiserikali za wilaya hiyo ambazo ni polisi (3), mahakama (2), Idara ya Ukaguzi wa Elimu, Ofisi ya Afisa Elimu Msingi (DEO) na Ofisi ya Mshauri wa Mgambo ambayo imepewa kompyuta moja.
Kishosha alisema vikundi 18 vya kijamii vya wilaya navyo vimenufaika na msaada huo, na kuvitaja vifaa vingine vilivyotolewa na chuo hicho kuwa ni cherehani ya ngozi na tanki la kuhifadhia maziwa ambavyo vimetolewa kwa kikundi cha nyota.
“Vifaa vyote hivyo vyote pamoja na kinanda kikubwa ambacho kimetolewa kwa Kanisa Katoliki Sub Parish ya Kolomije, vina thamani ya zaidi ya sh milioni 200,” alisema.
Akipokea msaada huo, Kitwanga aliushukuru uongozi wa chuo hicho na kusema misaada hiyo ni kwa ajili ya kusaidia jamii na si kwa matumizi ya watu binafsi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa