Home » » Wasimamishwa masomo kwa kuchoma shule

Wasimamishwa masomo kwa kuchoma shule


na Stella Ibengwe, Sengerema
MKUU wa Wilaya ya Sengerema, Karen Yunus, amelazimika kuifunga shule ya wavulana ya Sengerema baada ya kutokea vurugu kubwa shuleni hapo zilizosababishwa na wanafunzi  wa kidato cha sita.
Vurugu hizo zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali za shule hiyo ikiwa ni kuteketezwa moto na kushambuliwa kwa mawe nyumba nane za walimu.
Wanafunzi hao walifanya vurugu hizo juzi usiku saa mbili muda mfupi baada ya kumaliza kula chakula cha usiku na ndipo wakawashawishi wenzao wa kidato cha tano washiriki kufanya vurugu hizo jambo ambalo hawakuliafiki.
Vurugu hizo zilidumu kwa muda wa saa moja na kisha kuzimwa na Jeshi la Polisi baada ya kufika eneo la tukio. Na jana mkuu wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, aliifunga shule hiyo hadi Julai 16 mwaka huu.
“Kutokana na kuwepo kwa uvunjifu wa amani kati ya walimu na wanafunzi na mali kuharibiwa...kuanzia sasa natamka kuifunga shule hii mpaka Julai 16,’’ alisema Yunus.
Mkuu wa shule hiyo, Zakaria Kahema, alisema dalili za kutokea vurugu hizo zilianza kujitokeza asubuhi wakiwa mstarini wakiimba wimbo wa shule.
Kwamba waliimba kwa sauti ya chini hali ambayo ilionyesha utovu wa nidhamu na baada ya kiranja wa zamu kuwaamuru kuongeza sauti walikaidi agizo hilo hatua ambayo ilipelekea kupewa adhabu.
Mali za shule zilizoharibiwa katika vurugu hizo ni nyumba nane za walimu ambazo zilivunjwa vioo kwa mawe na kuharibiwa mita za umeme sanjari na kuteketeza kwa moto duka la vifaa vya kujifunzia (stationery).
Alisema kuwa duka hilo la mwalimu Jonas Waziri, lilikuwa na komputa tatu, mashine za kutolea nakala mbili, printa mbili na vitu vingine, vyote vikiwa na thamani ya sh milioni 20.7 .
“Tutafanya tathmini ili kupata thamani halisi ya mali zote zilizo haribiwa na baada ya hapo tutawataarifu ila kwa sasa bado ni  mapema sana kusema,’’ alisema Kahema.
Nao  wanafunzi wa kidato cha sita waliosababisha vurugu hizo walisema kuwa walichukua hatua hiyo kutokana na uongozi mbovu wa serikali ya wanafunzi ikishirikiana na uongozi wa shule na hivyo kushindwa kutekeleza kero zao kwa muda mrefu licha ya kuwepo na mazungumzo kupitia vikao vyao.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa