Home » » DC awashukia wasiowalipa wakulima wa pamba

DC awashukia wasiowalipa wakulima wa pamba


na Berensi Alikadi, Bunda
MKUU wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, amepiga marufuku makampuni yanayodaiwa na wakulima wa pamba kutonunua pamba msimu huu hadi watakapolipa madeni ya misimu iliyopita.
Akiwahutubia wananchi wa mji wa Bunda jana katika viwanja vya stendi ya zamani ikiwa ni sehemu ya mkutano wake wa kwanza wa kujitambulisha kwa wananchi baada ya kuteuliwa hivi karibuni, alisema makampuni hayo yasipowalipa wakulima serikali wilayani Bunda itawachukulia hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Mkuu huyo wa Wilaya (DC), alisema wao katika soko la dunia hawakopeshwi pamba, lakini kwa nini wao wawakope wakulima na mbaya zaidi hawataki kuwalipa.
Aidha, alimuagiza Mkuu wa Polisi wilayani Bunda, Peter Ouma, kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani maofisa wote wa serikali na mawakala waliohusika kuhujumu pembejeo za kilimo wilayani Bunda kama ilivyoagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa, hivi karibuni.
Mirumbe aliwashauri wakulima kuongeza bidii katika kilimo cha pamba kwa kuwa ndilo zao pekee la biashara kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na inachangia pato kubwa katika mfuko wa taifa na kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na mikoa mingine inayolima zao hilo.
Kwa upande wao, wananchi wa mji wa Bunda wameipongeza hatua hiyo ya mkuu wa wilaya, kwani kama wanunuzi hao wakibanwa ipasavyo na kulipa madeni hayo pesa hizo zitawasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa