Home » » Jiji Mwanza lajivunia usafi

Jiji Mwanza lajivunia usafi


na Sitta Tumma, Mwanza


HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza, imesema ipo tayari kushiriki kinyang’anyiro cha usafi wa mazingira katika majiji ya nchi za Afrika Mashariki na Kati, pamoja na mataifa mbalimbali ya Ulaya, kwani jiji hilo limejizatiti kwa usafi.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, alisema hayo juzi ofisini kwake alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu siri ya mafanikio ya jiji hilo kuongoza miaka saba mfululizo kwa kushika nafasi ya kwanza katika usafi wa mazingira nchini.
Alisema mafanikio ya usafi huo wa mazingira yaliyofikiwa na jiji hilo yamechangiwa zaidi na elimu muhimu waliyoitoa kwa jamii ya jiji na viunga vyake, ushirikiano mzuri baina ya wadau, wananchi na vikundi mbalimbali vya usafi.
Sababu nyingine aliitaja kuwa ni kuwepo kwa sheria ndogo za jiji hilo, zinazoruhusu kukamatwa kwa mtu yeyote anayepatikana na kosa la kutupa ovyo takataka ndani ya jiji, na kwamba adhabu mbalimbali zimekuwa zikitolewa ikiwa ni pamoja na kutozwa faini isiyozidi sh 50,000 papo hapo, au kufikishwa mahakamani kwa mtu aliyekamatwa akichafua mazingira.
Alisema iwapo serikali itaona umuhimu wa majiji, manispaa na halmashauri zake kushiriki katika kwenye kinyang'anyiro cha usafi kwa mataifa ya nje ya nchi, Jiji la Mwanza halitarudi nyuma kushiriki na lina uwezo wa kushika nafasi ya juu na hatimaye kukosa wapinzani.

Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa