Home » » Miaka 60 jela kwa kukutwa na nyara za serikali

Miaka 60 jela kwa kukutwa na nyara za serikali


Na Berensi Alikadi, Bunda
MAHAKAMA ya wilaya ya Bunda jana imehukumu kifungo cha miaka 60 jela watu watatu baada ya kupatikana na hatia ya makosa mbalimbali ikiwemo kupatikana na nyara, kuingia hifadhini bila kibali na kukutwa na silaha bila kibali ndani ya hifadhi.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Inocent Amosi (25), Joseph Lazaro (18) na Emanuel Juma (16) wote wakazi wa kijiji cha Kunzugu, kata ya Kunzugu katika mamlaka ya mji mdogo wa Bunda, mkoani Mara.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya hiyo, Joachim Tiganga, ilidaiwa na mwendesha mashtaka wa kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya Serengeti, Prochas Longoma, kuwa mnamo Juni 25 mwaka jana, majira ya asubuhi, washtakiwa kwa pamoja walikamatwa na askari wa hifadhi ya Serengeti.
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao walikutwa wakiwinda ndani ya hifadhi, wakiwa na silaha na pia wakiwa na wanyama watatu aina ya pundamilia bila kibali cha mkurugenzi wa wanyama pori.
Akiwasomea hukumu hiyo hakimu Tiganga alisema kuwa mahakama hiyo imeridhika pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka mahakamani hapo na hivyo akawahukumu kila mmoja katika kosa la kwanza kila mmoja alitakiwa kulipa faini ya sh 20,000 au kifungo cha miezi sita.
Katika kosa la pili washtakiwa wote walihukumiwa kila mmoja kulipa faini ya sh 30,000 au kifungo cha mwaka mmoja na katika kosa la tatu washtakiwa wote walitiwa hatiani kila mmoja kifungo cha miaka mitatu jela ambapo katika kosa la nne washtakiwa wote walitiwa hatiani kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20 na kwamba adhabu hizo zitaenda sambamba.

Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa