Home » » CCM, Chadema watwangana mawe

CCM, Chadema watwangana mawe

 Polisi wawatawanya kwa mabomu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow
Jeshi la Polisi jijini Mwanza limelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa vyama vya Chadema na CCM waliokuwa wakishambuliana kwa kurushiana mawe baada ya kumalizika kampeni za vyama hivyo zilizofanyika katika maeneo tofauti ya Kabuhoro na Mwembesangara kwa ajili ya uchaguzi wa udiwani Kata ya Kirumba jijini hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alithibitisha askari wake kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi hao kwa lengo la kurejesha amani na kuepusha uharibifu wa mali.
“Ni kweli polisi tulilazimika juzi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa CCM na Chadema baada ya kuanza kurushiana mawe katika eneo la Kirumba karibu na hoteli ya La Kairo, lakini tunashukuru hakuna uharibifu mkubwa wa mali uliotokea,” alisema Kamanda Barlow.


Aliongeza: “Ni kijana mmoja tu anayedhaniwa kuwa mfuasi wa Chadema ambaye alionekana kushindwa kuzungumza pengine kutokana na kukanyagwa lakini alipopelekwa hospitalini aliondoka hata kabla ya kupatiwa matibabu,” alisema.
Aliwaonya wafuasi wa vyama vyote kufanya kampeni za kiungwana kwani Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua  watakaoshiriki katika vurugu za aina yoyote.
Hata hivyo, Chadema kimewashutumu wafuasi wa CCM kuwa ndiyo waliowavamia wafuasi wao waliokuwa wakitokea katika mkutano wa kampeni uliokuwa ukifanyika eneo la Kabuhoro.
Diwani wa Kata ya Nyamanoro (Chadema), Abubakar Kapera, alidai  kwamba, wafuasi wa chama hicho walikuwa wakitokea kwenye mkutano uliofanyika eneo la Kabuhoro, lakini wakati wakirejea majumbani wakiwa katika kundi kubwa walipofika eneo la Hoteli ya Moon Light karibu na ofisi za CCM Kata ya Kirumba, wafuasi wa chama hicho waliwavamia na kuanza kuwarushia mawe.
Alisema Chadema kinafanya kampeni zake bila vurugu lakini hawatasita kujibu mapigo iwapo watachokozwa na iwapo Jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla watashindwa kutenda haki kwa vyama vyote.
Na katika hatua nyingine, Katibu Mkuu (Chadema),  Dk. Willibrod Slaa, amemtuhumu Rais Jakaya Kikwete, kwamba ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, ahakikishe anampatia zawadi ya kiti cha udiwani kata ya Kirumba.
Dk. Slaa alitoa madai hayo juzi wakati akimnadi mgombea wa udiwani kata ya Kirumba, jijini Mwanza kupitia Chadema, Bahati Kahungu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Bujumbura.
Alidai kuwa, amepata taarifa kwamba Rais Kikwete alimpigia simu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na kumwambia kwamba zawadi anayohitaji kutoka kwake ni Diwani wa Kata ya Kirumba kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Ndugu wananchi, hili ni jambo la kushangaza kidogo, yaani diwani hivi sasa siyo tena msimamizi wa demokrasia, siyo tena msimamizi wa maendeleo, bali ni zawadi kwa Kikwete,” alisema Dk. Slaa.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa, alidai ana taarifa za upotevu wa takribani Sh.  milioni 240 katika Idara ya Elimu ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Aliwataka madiwani na wabunge wa Chadema katika halmashauri hiyo kufuatilia kwa karibu na kuwabana watumishi waliohusika na upotevu wa fedha hizo za wananchi.
Aliwaonya madiwani na wabunge wasikubali kuhongwa vijisenti ili wanyamazie upotevu huo wa fedha za wananchi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa Chadema alitumia mkutano huo wa kampeni za udiwani kata ya Kirumba kuwataka madiwani na wabunge wa chama hicho  katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha wanapeleka kwa wananchi taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
“Ninawaagiza madiwani na wabunge wa Chadema kuhakikisha mnapeleka taarifa kwa wananchi kupitia mbao za matangazo au katika mikutano ya hadhara kama huu,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo na kuomba kura kwa wananchi, mgombea udiwani kata ya Kirumba, Bahati Kahungu, alisema akichaguliwa atashughulikia matatizo yaliyokithiri katika kata hiyo ambayo ni maji, ubovu wa barabara na makazi yasiyopimwa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa