Tone

Tone
Home » » Wanazuoni watabiri Ukawa kuidhibiti CCM

Wanazuoni watabiri Ukawa kuidhibiti CCM

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wanazuoni mahiri nchini wameelezea kuimarika kwa upinzani kumejenga ushindani mkubwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja na Mkurugenzi mtendaji wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, (pichani) wamesema hayo kwa nyakati tofauti walipohojiwa kuhusu hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi huo.

Dk. Semboja alisema ushindani wa kisiasa uliopo sasa unaweza kuifanya nchi kuwa na serikali ya mseto baada ya uchaguzi mkuu wa  mwaka huu. Alisema ushindani huo utawawezesha wagombea wengi kuchaguliwa kutokana na kuaminiwa kwao na si kwa sababu ya vyama vinavyowateua.

Mtaalamu huyo wa masuala ya siasa alisema, moja ya sababu ya kushamiri kwa nguvu za upinzani ni kasoro zilizojitokeza katika mchakato wa kumpata mgombea urais na ubunge kupitia CCM.

“Umekuwa mchakato wenye kila dalili za kukomoana, hatua ambayo imeleta mianya mingi ya kugawa kura za wagombea wa CCM akiwamo wa urais ambaye Dk. John Magufuli,” alisema.

Dk Semboja alisema kwa upande wa Ukawa, hatua ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kuwania urais, kumetoa changamoto kubwa na kuongeza nguvu za upinzani.

Akizungumzia kushindwa kwa baadhi ya mawaziri wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika kura za maoni, Dk. Semboja alisema ni ishara za kutokuwa na uwezo katika uongozi wa umma.

Naye Kijo-Bisimba, alisema kushindwa kwa baadhi ya mawaziri katika kura za maoni kumetokana na uelewa wa wananchi kuhusu uongozi wa umma unaojali maslahi yao.

Alisema wananchi walitarajia waliokuwa madarakani wangetekeleza wajibu wao ipasavyo na ilipokuwa tofauti na matarajio hayo, waliamua ‘kuwapiga chini’.

“Watu hawawezi kuwa mbumbumbu siku zote, wananchi wameamka hata ukienda vijijini watu wanajua haki zao na wamchague nani aweze kuwatetea…hii imetokana na elimu ya uraia pamoja na kuwapo matukio mbalimbali yakiwamo ya ufisadi wa Tegeta Escrow,” alisema Dk. Bisimba.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa