Home » » MBUNGE KWIMBA AMLIPUA DIWANI KUTOFANYA VIKAO VYA MAENDELEO KWENYE KATA

MBUNGE KWIMBA AMLIPUA DIWANI KUTOFANYA VIKAO VYA MAENDELEO KWENYE KATA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

NA PETER FABIAN-KWIMBA.-G SENGO BLOG
MBUNGE wa jimbo la Kwimba mkoani Mwanza, Shanif Mansoor (CCM), amemripua Diwani wa Kata ya Mwankulwe, Malando Sanduli (CCM) kuwa ameshindwa kufikisha kero za wananchi kwenye vikao vya Halmashauri ya wilaya ya Kwimba.
Pia ameshindwa kuitisha vikao vya Kamati ya Meendeleo ya Kata (WDC) na kusababisha kukwama kwa miradi mbalimbali ya maendeleo Katani humo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Luhala Katani humo juzi, baada ya baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho kulalamikia ubovu wa barabara za Mwankulwe- Luhala-Malampaka na Ikunda –Bugunga uliokithiri na kutopitika kwa urahisi, Shanif alisema Diwani huyo hawezi kuwaletea maendeleo.
“Diwani wenu kama hana muda wa kuwatumikia angeachia wengine wawaongoze maana nimefika mara tatu katika Kata hii lakini haonekani, kila nikimpigia simu anasema yuko bize nije niwasikilize, hata kero moja ya barabara hizi hajaipeleka Halmashauri na hahudhurii vikao vya Baraza,” alisema.
Mansoor alieleza kwamba, barabara hizo hazikubaliki na kuwaomba wananchi wa Kata hiyo awamu ijayo wachague mwakilishi mwingine kutoka CCM anayeweza kuwatumikia kikamilifu badala ya kumchagua tena Sanduli.
Alieleza kwamba, pamoja na diwani huyo kutojali kero za wananchi, baada ya kupata taarifa za kero mbalimbali za Kata hiyo ikiwemo kukosekana kwa Zahanati katika Vijiji vya Luhala na Bugunga, alipeleka mifuko 100 ya saruji na tayari ujenzi wa Zahanati ya Luhala umeanza.
Mansoor pamoja na kuahidi kuongeza saruji nyingine kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati hiyo, alisema suala la diwani huyo atalifikisha kwenye uongozi wa CCM wilayani Kwimba na kufikisha kero ya barabara hizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili zitatuliwe.
“Nashangaa kuwa Diwani huyu anazunguka jimboni kuwapigia debe watu wanaotaka kuwania ubunge wakati yeye Kata yake imemshinda, nawaombeni wananchi mniunge mkono kwa kunichagua tena wakati ukifika na mnichagulie Diwani mchapa kazi kutoka CCM tutatue kero zenu kwa pamoja,” alielea kuwa atafikisha na kuwashauri viongozi kuangalkia mwenendo na jinsi diwani huyo anavyozuia maendeleo..
Katika mkutano huo baada ya kuzindua kisima cha Ikunda, alikabidhi vyerehani viwili kwa wajasiriamali, sh 300,000 kwa ajili ya ununuzi wa baiskeli za Wauguzi wawili wa afya Katani humo na zaidi ya sh 2.5 kuwezesha vikundi vya wajasirimali vya Luhala, Ikunda na Bugunga.
Aliwataka wananchi wa Kata hiyo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka na watakaoshirikiana kuwaletea maendeleo kwani wakikosa fursa hiyo hawataweza kuwachagua.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa