Tone

Tone
Home » » MADEREVA WAMESIKILIZWA, NAO WASAIDIE KUDHIBITI AJALI

MADEREVA WAMESIKILIZWA, NAO WASAIDIE KUDHIBITI AJALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KATIKA siku za hivi karibuni kuna mambo makubwa mawili yamejitokeza katika sekta ya usafirishaji, hususani usafiri wa barabarani na kuliweka Taifa katika tafrani kubwa.
Mambo hayo mawili ni kutokea kwa ajali nyingi za barabarani zilizohusisha mabasi kadhaa na kusababisha vifo vya makumi ya Watanzania wasio na hatia, na jambo la pili ni kutokea kwa mgomo wa madereva.
Matukio hayo yanayoonekana kushabihiana kwa aina fulani yaligeuka kuwa kero kubwa kwa wananchi na kuliweka Taifa katika hali tete.
Katika matukio ya ajali za barabarani, Watanzania wameshuhudia ndugu zao wakifa katika ajali za mabasi ya Ngorika, Ratco, Happy Nation, Nganga na mengineyo kutokana na sababu ambazo zingeweza kuepukika.
Lakini wakati matukio ya ajali yakishamiri, madereva wa mabasi ya abiria nchini yakiwemo yale yaendayo mikoani na yale yatoayo huduma hiyo katika miji wakagoma, kupinga maelekezo kadhaa ya serikali.
Mojawapo ya mambo waliyogomea ni agizo la kuwataka kurudi shule kusoma kila wanapoomba leseni ya daraja fulani. Lengo la serikali likiwa ni kuhakikisha kuwa kila dereva anapata daraja la leseni kulingana na kiwango fulani cha elimu.
Lakini kwa bahati mbaya sana, serikali ikaweka kipengele cha ada kuwawezesha madereva hao kupata kiwango hicho cha elimu kinachotakiwa, bila kuangalia uwezo na mazingira ya kazi ya udereva, hatua iliyozua sokomoko.
Kwetu sisi pamoja na kukubaliana na hoja za pande zote mbili, tunaunga mkono maafikiano yaliyofikiwa na pande husika kwani ni kutokana na maafikiano hayo ndio maana huduma za usafiri zimerejea katika hali yake ya kawaida.
Hata hivyo rai yetu katika hili ni kuwaomba madereva na wadau wote wanaohusika na usafiri wa barabarani, kutafuta mbinu za kuzuia ongezeko la ajali za barabarani.
Ni kweli kwamba ongezeko la ajali hizo linasababishwa na mambo mengi na si tu kiwango cha elimu kwa madereva, lakini kwa namna yoyote ile ni lazima suala la ajali hizo lipatiwe ufumbuzi haraka ili kuokoa maisha ya nguvu kazi ya taifa.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka ametangaza serikali kuondoa hoja zake zote, suala la madereva kurejea kwenye mafunzo, suala la tochi za barabarani na masuala mengine kulingana na hoja za madereva lakini kukubaliwa kwa hoja hizo kuwe chachu kwa madereva nao kutii sheria za usalama barabarani.
Kama sheria za barabarani zitafuatwa itakiwavyo, hakuna ubishi kwamba ajali zitapungua na hilo likiwezekana, hakutakuwa na umuhimu wa madereva kwenda shule wala kuwepo kwa tochi za kupima mwendo kasi kama madereva wanavyojaribu kushinikiza.
Lakini kama ajali zitaendelea kwa kasi tunayoiona sasa, ni ushauri wetu kwa wadau wote wa usafiri wa barabarani kukaa chini na kuangalia mikakati mbadala ya kudhibiti hali hiyo haraka sana ili kuokoa uhai wa watumiaji wa barabara zetu.
Chanzo:Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa