Home » » HII SIYO LUGHA YA TAIFA

HII SIYO LUGHA YA TAIFA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


MWAKA 2011 wakuu wa nchi yetu waliamua kwamba watasherehekea miaka 50 ya uhuru wa kitu fulani, lakini wakashindwa kusema ni kitu gani walikuwa wanasherehekea.
Baadhi ya maandiko yaliyotangazwa wakati huo yalisema kwamba ni sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Tanzania, lakini sote tunajua kwamba hakuna nchi iliyoitwa Tanzania iliyopata uhuru wake mwaka 1961. Baadhi yakasema kwamba ni miaka 50 ya uhuru wa “Tanzania Bara”, lakini tunajua vile vile kwamba hakuna nchi iliyoitwa Tanzania Bara iliyopata uhuru mwaka 1961.
Kwamba wakuu wetu walishindwa kusema ni kitu gani kilitokea tarehe 9 Desemba 1961 ni kielelezo cha tatizo kubwa tulilo nalo katika kujenga utaifa wetu. Tunajifunga ndani ya ujinga tunapokataa kusema ukweli kwamba mwaka 1961 hakukuwa na nchi iliyoitwa Tanzania. Kilichokuwapo ni nchi iliyoitwa Tanganyika ikiwa chini ya himaya ya Uingereza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa.
Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1961 na miaka mitatu baadaye ikaungana na Zanzibar kuunda kile kilichokuja kuitwa Jamuhuri ya Muungano wa (ya) Tanzania.
Hili nalisema ili kuondoa utando uliofunika tafakuri zetu, utando ambao unatuelekeza kujifanyia mambo kwa kubabaisha tu, bila kujisumbua kufikiri angalau kidogo. Tungewekeza kidogo katika tafakuri kuhusu historia yetu, tungekuwa na nia ya kweli ya kuienzi nchi yetu na watu wake, tungekumbuka kwamba nchi hii (angalau ile sehemu ya nchi yetu inayoitwa ‘Bara’) ilikuwa inaitwa Tanganyika, na ilikuwa na utambulisho wake katika jitihada za kujenga taifa huru na linalojiheshimu.
Katika utambuzi huo tungewatambua mashujaa wetu wa kweli na kuwatuza kwa nishani wanazostahili. Kwa kuwa hatuko tena katika ujenzi wa utaifa ila kila mmoja wetu anatafuta kujijenga yeye na familia yake, haya tumeyasahau, na sherehe zetu za kuadhimisha hiki au kile zinakuwa ni fursa nyingine za watu kujitajirisha kwa kujipatia tenda za kutengeneza fulana au vitenge, ama za kuandaa hafla hii au ile.
Katika utafutaji huu, maana ya kweli ya shughuli yenyewe inakuwa ni ya mwisho kufikiriwa. Ndiyo maana katika kuwakumbuka wakuu mbalimbali, watu muhimu katika maisha yetu kama taifa lililokuwa likijijenga, tulijikuta tunatenda dhambi nzito. Inawezekana vipi, kwa mfano, kuwakumbuka ma-spika wa Bunge letu waliopita, kisha ukawataja Pius Msekwa na Anne makinda, lakini tukamshau Adam Sapi Mkwawa? Mimi sina ugomvi na waungwana hawa wawili, lakini katika kuwapima watu na mchango wao, tunaweza kweli tukatetea jambo kama hili? Kama si kukosa haya ni nini?
Tungekuwa tuna uwezo wa kuangalia tumefanya nini huko tulikotoka na kujifunza kutokana na makosa yetu ili tusiyafanye tena, tungejifunza kwamba hivyo sivyo mataifa yanavyokumbuka historia zake. Tungekuwa na busara za kuwakumbuka na kuwatunuku nishani watu waliofanya kazi ya kweli katika kutoa mchango wao katika ujenzi wa taifa tunalotaraji kujenga. Kumbuka nimesema mara kadhaa kwamba tunaweza kuwa na nchi lakini tusiwe na taifa.
Watu ambao nasema tungewakumbuka ni pamoja na hayati Shaaban Robert, ambaye katika kusherehekea miaka 50 (ya kitu fulani) hatukumsikia kabisa. Pamoja naye hatukuwasikia akina Kaluta Amri Abedi, Mathias Mnyampala, Akilimali Snowhite, Joseph Kiimbila, na wengine waliochangia katika makuzi na maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Najua kwamba si waandishi wa Kiswahili tu waliosahauliwa katika maadhimisho hayo ya miaka 50 (ya kitu fulani). Hatukuwasikia wanamichezo, wasanii, waalimu mashuhuri, wakulima mahiri. Lakini kutokuwapo kwa jina la Shaaban Robert miongoni mwa watu waliokumbukwa katika sherehe hiyo kulidhihirisha kwangu maana halisi ya sherehe hizo kama mahali pa kujikweza kwa baadhi ya watu na kutengeneza faida ya fedha kwa baadhi ya wengine. Ni sherehe zilizonyimwa heshima ambayo ingestahili.
Kwa nini Shaaban Robert si muhimu? Hivi tunaweza kufikiria kwamba Waingereza wanaweza kuadhimisha karne kadhaa za utaifa wao halafu wakawatunikia nishani wanasiasa na majemadari kadhaa waliopita lakini wakamsahau William Shakespeare, Goeffrey Chaucer au William Wordsworth?
Au Wafaransa wamsahau Moliere au Balzac, au Victor Hugo? Au Warusi wamsahau Alexander Pushkin au Lev Tolstoy ? Au Marekani wamsahau Mark Twain au John Steinbeck, au James Fenimore Cooper ? Haiwezekani.
Kwetu sisi inawezekana, kwa sababu waandishi wetu hawana umuhimu kwetu. Tungekuwa tunajenga taifa, kundi moja ambalo lingekuwa msitari wa mbele kabisa katika utambulisho wa utaifa huo lingekuwa ni kundi la waandishi wa lugha ya taifa. Tungewatambua kama viongozi wa utamaduni na fikra za kitaifa. Tungewaenzi. Hatuwaenzi kwa sababu hatujengi taifa, tunakubali na kufurahia kubaki tukiwa ni nchi tu, na kwa sababu hiyo hatuna lugha ya taifa. Kama hujengi taifa, huhitaji lugha ya taifa, na usipokuwa na lugha ya taifa huwezi kuwa na taifa.
Jinsi tunavyokitumia Kiswahili ni kama misemo inayotufanya tuwasiliane na kubadilishana mawazo katika shughuli nyepesi nyepesi, katika biashara ndogo ndogo, masihara, mzaha na utani, na siasa za porojo. Katika matumizi ya Kiswahili hakuna jambo makini linalofanyika ambalo tunalijadili kwa makini.
Siasa ndicho kielelezo kikuu cha nafasi ya Kiswahili katika nchi yetu. Siasa yetu ni uwanja wa masihara, upuuzi na vichekesho vya wasanii wachovu. Tumekwisha kuacha kutumai jambo la maana kutoka kwa wanasiasa isipokuwa kutufanya tucheke kwa huzuni. Hakuna wazo linalosanifiwa na kupangiliwa kwa weledi na likawasilishwa kwa werevu katika siasa zetu, kiasi kwamba siasa imekuwa na maana ya tamthilia isiyotarajiwa kuchukuliwa kwa uzito wowote.
Lugha ya taifa haina budi kutumika katika kuliendeleza taifa husika. Kuliendeleza taifa ina maana, kwanza ya kulifanya taifa liendelee kuwapo, lijiimarishe, lijiongezee uwezo wa kielimu, kisayansi, kiuchumi na kiutamaduni. Kwa maana hiyo, lugha ya taifa haina budi pia kuwa lugha ya elimu na sayansi na tafakuri.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa huko tulikotoka kwa maana kwamba taifa la Wasukuma liliwafunza vijana wa Kisukuma kwa Kisukuma. Viwango vya sayansi ya Kisukuma ya wakati huo ndivyo vilivyokuwa, na uwezo wa Wasukuma wa kuielewa dunia ndivyo ulivyokuwa, lakini kila walichojua walikirithisha kwa vizazi vipya kupitia lugha ya taifa lao, yaani Kisukuma.
Haiwezi kuwa tofauti katika taifa la kisasa. Hatuwezi kuwa na lugha ya taifa kwa sababu tu eti tuna Katiba inayotamka kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa, au sheria iliyotungwa na Bunge. Lugha ya taifa hujengwa kwa vitendo, hususan kwa kuitumia katika shughuli nzito kama elimu, sayansi teknolojia na tafakuri za kina.
Kiswahili, kama tunavyokitumia hivi sasa, ni ‘lingua franca, ’ lugha nyepesi ya kuelewana katika mambo madogo madogo yasiyokuwa na umuhimu mkubwa. Ni lugha ya kuuza na kununua mandazi na njugu.
Kuna wakati Kiswahili kilikuwa kwa kasi kubwa, na kikaimarika katika medani ya siasa. Kiswahili kilikuwa ndiyo nguzo kuu katika kujenga utaifa wa Watanganyika wa wakati wa kudai uhuru, na katika kujenga utaifa wa Watanzania kama mataifa mawili yaliyoungana. Lakini kwa sasa, Kiswahili kimedumaa na kinazidi kudumaa kwa sababu hakina jukumu la msingi la kutekeleza; tumekitelekeza.
Ndiyo maana tunaweza kukusanyana na kupeana nishani za miaka 50 (ya kitu fulani), lakini tukamsahau Shaaban Robert.

Chanzo:Raia Mwema

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa