Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza.
Mapacha hao walizaliwa Januari 3, mwaka huu katika Hospitali ya Mkoa ya Mara na baadaye kuhamishiwa katika Hospital ya Rufaa Bugando kwa matibabu zaidi.
Watoto hao waliozaliwa wakiwa na uzito wa kilo 4.6 kwa pamoja, wameungana vifua na matumbo.
Kwa mujibu wa Dk. Festo Manyama, daktari wa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, timu ya madaktari wa upasuaji na wataalam wengine, wamekusanyika kuamua namna bora ya kukabiliana na hali yao.
"Tunafanya kila liwezekanalo katika uwezo wetu ili kuokoa maisha ya watoto hawa," alisema.
Alisema kabla ya upasuaji, mapacha hao walitakiwa kupitia tomografia (CT) na kufanya kipimo cha Ultra Sound ili kujua kama watoto hao wameungana baadhi ya maeneo na viungo muhimu.
"Tumeshafanya kipimo cha Ultra Sound na kupata matokeo yanayoonyesha kuwa hakuna sehemu nyingine muhimu walizoungana, lakini tunahitaji kufanya vipimo vingine kwa kutumia mashine ya CT Scan, ambayo itatupatia hitimisho," alisema Dk. Manyama.
Alisema madaktari watafanya upasuaji endapo watoto hao hawatakuwa wameungana sehemu muhimu katika miili yao.
Kwa mujibu wa Dk. Manyama, watoto hao wanahitaji ufuatiliaji wa karibu wa daktari ili waepukana na magonjwa.
"Tunawapa dawa na kuwalinda na magonjwa ya kuambukiza, pia wanatumia mashine ya oksijeni kwa kupumua na mirija ya chakula,", aliongeza Dk. Manyama.
Alifafanua kuwa uongozi wa hospitali hiyo unatarajia kutoa rufaa ili watoto hao wapelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili.
"Tutawahamishia Hospitali ya Muhimbili kwa sababu hospitali yetu haina uwezo mkubwa wa kukabiliana na suala hili, lakini kwa wakati huu, tunafanya kila tuwezalo ili kuokoa maisha yao," alisema.
Mama wa mapacha hao, Hellena Paulo (20), ameiomba serikali kumuunga mkono ili kuhakikisha watoto wake wanapata huduma ya afya bora inayohitajika katika hali yao.
"Hofu yangu kubwa ni kwamba hospitali zetu hawataweza kukabiliana na hili, nimeambiwa upasuaji unaweza kufanyika nje ya nchi na mimi ni mama maskini, hivyo ninaomba serikali inisaidie," alisema Hellen.
Tanzania imekuwa ikishuhudia matukio kadhaa ya mapacha walioungana katika miaka ya hivi karibuni.
Mwishoni mwa mwaka jana, Hospitali ya Apollo ilitangaza kufanikiwa kutenganisha mapacha waliokuwa wameungana kutoka Tanzania katika upasuaji uliochukua saa 11 na wataalam 50.
Mapacha hao, Abriana na Adriana, walikuwa wameungana katika kifua chini ya tumbo, hali ya kitaalam inajulikana kama 'Thoraco Omphalopagus'.
Mapacha hao walitenganishwa baada ya mipango ya kina na ushirikiano kati ya madakitari bingwa wa mfumo wa mkojo, figo, ini na moyo na madakitari bingwa wa watoto.
Aidha, aliteuliwa daktari bingwa mmoja kama kiongozi wa timu ambaye alisimamia utaratibu mzima wa upasuaji.
Mapacha hao pia walikuwa wakitumia mvungu mmoja wa moyo na walikuwa wameungana ini.
Aidha, mwishoni mwa mwaka 2013, mapacha wengine wa kiume waliokuwa wameungana Ericana na Eluid kutoka Tanzania, walifanikiwa kutenganishwa na wataalam wa hospitali hiyo.
SOURCE:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment