JESHI la Polisi mkoani
Mwanza, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kumteka mtoto mwenye
ulemavu wa ngozi (albino), Pendo Emmanuel (4), mkazi wa Wilaya ya
Kwimba, mkoani humo.
Miongoni wa watuhumiwa hao ni baba mzazi wa mtoto huyo ambaye alitekwa Desemba 27 mwaka huu, saa 4:30 usiku katika Kijiji cha Ndami, Tarafa ya Mwamashimba.
Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Valentino Mlowola, alisema mtoto huyo kabla ya kutekwa,watekaji walivunja mlango wa nyumba yao kwa jiwe la fatuma.
Alisema wakati mlango unavunjwa, mtoto huyo alikuwa amelala chumbani na kaka yake, mama na mtoto mchanga ambapo baba yao alikuwa amelala sebuleni.
“Baada ya mlango kuvunjwa, watekaji waliingia ndani na kumweka chini ya ulinzi, Emmanuel Shilinde ‘Nundi’ (28), baba yao mzazi, kumchukua Pendo na kuondoka naye wakitumia usafiri wa pikipiki,” alisema.
Aliongeza kuwa, Polisi walipata taarifa na kufika eneo la tukio katika kijiji hicho ambacho kipo mpakani mwa Wilaya ya Kwimba na Misungwi saa 7:30 usiku.
Kamanda Mlowola alisema, hadi sasa mtoto huyo hajapatikana lakini jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliofanya kitendo hicho na mahali alipo mtoto.
“Hadi sasa tunawashikilia watu wanne akiwemo baba mzazi wa mtoto aliyetekwa ambao wanaendelea kuhojiwa ili kupata ukweli wa jambo hili, tayari kikosi cha makachero kutoka Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam, kimewasili hapa Kwimba ili kuongeza nguvu,” alisema.
Alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, inawaomba wananchi kutoa ushirikiano ambao utafanikisha kupatikana kwa mtoto huyo akiwa hai.
“Matukio haya hapa Mwanza yalipungua sana, sasa yanaanza kurudi tena...hili ni tukio la kwanza mwaka huu, tunawaomba viongozi wa dini waendelee kuwajenga kiimani waumini wao ili waache vitendo hivyo kwani Serikali pekee haiwezi kumaliza tatizo hili bila wananchi,” alisema.
Alisisitiza kuwa, jeshi hilo litatumia rasilimali zake zote kuhakikisha wahusika wanapatikana akiwemo mtoto huyo akiwa hai na kutangaza zawadi ya sh. milioni tatu kwa mtu yeyote ambaye atafanikisha kupatikana kwa watu hao.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment