Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ZAIDI ya wanawake 600 mkoani Mwanza, wanatarajiwa kupata elimu juu
ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, uwekaji akiba pamoja na mafunzo ya
afya bora katika viwanja vya Mwaloni Kirumba Septemba 4 na 5 mwaka huu.
Kina mama na vijana kutoka Wilaya za Magu, Ilemela, Misungwi na
Nyamagana, wanatarajiwa kushiriki katika kampeni hiyo itakayotolewa na
taasisi ya Angels Moments ya jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Mwanza jana, Mkurugenzi
wa Taasisi ya Angels Moments, Naima Malima, alisema kampeni hiyo
inalenga kuwajengea uwezo na ujuzi wa kusimamia fedha zao kwa lengo la
kunyanyua uwezo wao wa kiuchumi pamoja na familia zao.
Naima, alisema kampeni hiyo imeanzia mkoani Mwanza kwa kutambua
fursa zilizopo mkoani humo, hivyo wanawake wa Mwanza watapewa elimu ya
msingi ya kibiashara na kuchochea namna ya kuchangamkia fursa mbalimbali
za kiuchumi zilizopo ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza.
“Kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na taasisi
ya Wama, tunatarajia kuwafikia wanawake wa vikundi vyote vya kijamii,
Saccos, Amcos, Vicoba na makundi mengine ya kijamii yanayojihusisha na
wajasiriamali na hivyo kampeni hii itawawezesha kujiongezea uwezo wa
kupata wateja wa bidhaa na huduma zao na kujitangaza zaidi,” alisema
Naima.
Aidha, alisema pamoja na Mkoa wa Mwanza, kampeni ya Mwanamke na
Uchumi pia itafanyika Tanga, Kigoma, Dodoma, Pwani, Ruvuma na Lindi
kuanzia mwishoni na mwanzoni mwa Septemba hadi Januari mwakani.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment