Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KATA ya Lamadi iliyopo katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu,
imetumia sh 734,415,500 kati ya mwaka 2011 na 2014 kwa ajili ya
shughuli mbalimbali za ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mdogo wa Lamadi jana,
Diwani Emmanuel Desela alisema fedha hizo zilizotolewa na serikali kuu,
wafadhili, mbunge wao Dk. Titus Kamani na nguvu kazi ya jamii,
zimetumika kwenye miradi ya maendeleo.
Desela aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa ofisi za serikali za
vijiji, madarasa, vyoo na ofisi za walimu katika shule mbalimbali za
msingi na sekondari, ukarabati wa jengo la OPD na ujenzi wa wodi ya
wazazi katika kituo cha afya Lukungu.
Alisema miradi mingine ni ujenzi wa kituo kipya cha mabasi cha
Lamadi, ujenzi wa maabara na utawala katika Shule ya Sekondari Lamadi,
ujenzi wa Shule ya Msingi Lamboni na ukarabati wa madarasa kwa shule za
msingi.
Aliitaja miradi mingine ni ujenzi wa madarasa ya awali katika Shule
ya Msingi Lukungu, usafi wa mazingira katika Mto Lamadi, mradi wa maji
wa Lamadi na Lukungu na kuimarisha barabara iendayo Ziwa Victoria.
Alisema kuna miradi ambayo haijatekelezeka kutokana na serikali
kushindwa kupeleka fedha kwa wakati huku akiitaja kuwa ni ujenzi wa
ofisi ya mtendaji wa Kata ya Lamadi, ujenzi wa soko kuu la mji huo
ambalo tayari limeshapimwa na upimaji wa viwanja.
Kwa mujibu wa diwani huyo, licha ya nguvu hiyo, wanazo changamoto
zinazowafanya washindwe kukamilisha miradi kwa wakati ikiwemo malumbano
ya kisiasa yanayowagawa wananchi.
Changamoto nyingine ni viongozi na watendaji kutokuwa makini katika
kusimamia fedha za serikali na wanyama waharibifu wanaotoka kwenye
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuharibu mazao ya wananchi na kusababisha
watu kukosa nguvu ya kuchangia.
Hata hivyo, aliweka wazi mikakati yao kuwa ni kuiomba serikali kuu
kuleta fedha za maendeleo kwa wakati, kuwashauri wanasiasa waache
kuwachanganya wananchi ili wafanye shughuli za maendeleo, viongozi na
watendaji kuwa makini katika kusimamia fedha za maendeleo na kujenga
kambi ya kuzuia wanyama waharibifu katika Kijiji cha Lukungu.
Wakati huo huo, juzi mkutano uliokuwa umeandaliwa na diwani huyo
katika mji mdogo wa Lamadi wenye vijiji viwili ili kuwasomea wananchi
taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, haukufanyika kutokana na
wananchi kutokujitokeza kwenye mkutano huo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment