Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
Makada hao ni wale walioadhibiwa kwa kupewa onyo kali na kuwekwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja kwa kuanza kampeni mapema za kutafuta kuteuliwa kugombea urais mwaka 2015, kinyume cha utaratibu na mwongozo wa chama.
Hao ni pamoja na waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Wote waliitwa Dodoma na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili kuhusu madai ya kuanza kampeni mapema zinazodaiwa kuivuruga CCM na wanachama wake nchini.
Habari ambazo NIPASHE imezipata zinaeleza kuwa licha ya kutolewa kwa adhabu hiyo, kumekuwapo na madai ya upendeleo wa wazi wa kuwaruhusu baadhi ya makada kuendelea na kampeni, huku wengine wakibaguliwa.
Madai hayo, ambayo yametolewa na viongozi hao wa wafanyabishara, yanahusisha ugeni rasmi wa Waziri Membe aliokuwa nao wakati wa uzinduzi wa albamu ya “I Love Mwanza takribani wiki mbili zilizopita ”.
Walisema hali hiyo hali hiyo ni uthibitisho wa dhahiri wa madai ya upendeleo, ambao Waziri Membe anadaiwa kufanyiwa.
Inaelezwa kuwa wakati Waziri Membe akifanya shughuli hiyo iliyoambatana na mbwembwe za hali ya juu, Lowassa alizuiwa kufanya harambee jijini Mwanza.
Waziri Membe katika uzinduzi huo aliwezesha filamu hiyo kununuliwa na wadau kwa zaidi ya Sh. milioni 50. Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, jijini humo.
Juzi wafanyabiashara hao watano walionekana wakibarizi baadhi ya mitaa mjini hapa, wanne kati yao wakiwa wamevaa fulana zenye rangi ya njano, zikiwa na andiko linalosomeka: “MIMI NI NURU YAKO.”
Awali, walikutana na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Thobias Mwilapa, kwenye makao makuu ya chama hicho, ambaye hata hivyo, mbali na kuthibitisha kupokea ugeni huo, alikataa katakata kuzungumzia ujumbe waliowasilisha kwake.
“Mimi ni ofisa na siyo msemaji wa chama. Kama una lolote unalohitaji kufahamu wasiliana na wasemaji wa chama, mheshimiwa Nape (Nnauye) au Katibu Mkuu mwenyewe,” alisema Mwilapa.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema hakuwa na taarifa juu ya ujio wa wanachama hao kutoka mkoani Mwanza.
Alipotakiwa na mwandishi kuelezea ukweli wa sababu zilizowafanya wanachama hao kwenda Dodoma, Nape alisema:
“Nakuheshimu sana, lakini siwezi kuzungumzia mambo, ambayo siyafahamu. Hao vijana (wafanyabiashara) mimi sijawaona na wala sijaletewa taarifa yoyote kuhusu hayo unayoniuliza. Nimekuwa nikitumika vibaya kitu, ambacho mimi sipendi.”
Wakizungumza na NIPASHE kwenye Mtaa wa Jamatini, mjini hapa jana, vijana hao walithibitisha kuwa wao ni viongozi wa wafanyabiashara, ambao ni wanachama wa CCM, lakini walikataa kueleza sababu za ujio wao.
“Sisi tumekuja kisiasa. Tuna maadili yanayotuongoza. Kilichotuleta kimewasilishwa kwa viongozi wetu. Kama kuna kinachotakiwa kuzungumzwa kupitia vyombo vya habari, wao watazungumza. Tusamehe sana hatutaweza kueleza chochote,” alisema mmoja wao.
Hata hivyo, taarifa zilizolifikia NIPASHE wakati tunakwenda mitamboni jana zilieleza kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wakijiandaa kwenda jijini Dar es Salaam kukutana na Kinana kwa madai kwamba, majibu waliyopewa Dodoma hayakuwaridhisha.
Februari 13, mwaka huu sekretarieti ya CCM ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula na Kinana ilianza kuwahoji makada hao juu ya kuanza kampeni mapema.
Februari 19, mwaka huu, Kamati Kuu ilitangaza adhabu kwa makada hao baada ya kuridhika kwamba walianza kampeni mapema kinyume cha taratibu za chama hicho.
Wote walizuiwa kwa mwaka mmoja kujihusisha na shughuli za chama. CCM pia kilisema kuwa kitaendelea kuwafuatilia na atakayebainika atachukuliwa hatua zaidi.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment