Home » » RAIS SERIKALI YA WANAFUNZI CUHAS ATOWEKA KIUTATANISHI

RAIS SERIKALI YA WANAFUNZI CUHAS ATOWEKA KIUTATANISHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Valentino Mlowola
 
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Bugando (Cuhas), mkoani Mwanza, Musa Mdede, anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, katika tukio linalosadikiwa kuwa ni la utekaji nyara.
Mdede, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), anadaiwa kupotea muda mfupi jana wakati akijiandaa kwenda kurudisha fomu za kuomba kutetea nafasi yake katika uchaguzi wa viongozi wa serikali hiyo.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika katika chuo hicho, Juni 29, mwaka huu.

Katika uchaguzi huo, Mdede anapambana na wagombea wengine wawili wanaowania nafasi hiyo.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi hao, Benjamin Thomas, alithibitisha Mdede kukumbwa na masaibu hayo na kusema hadi jana jioni hawakuwa na taarifa zozote kuhusu aliko.

Alisema kutokana na hali hiyo, kwa kushirikiana na Mshauri wa Wanafunzi wa Chuo hicho, Kastar Mapunda, walikwenda katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mwanza na kutoa taarifa kuhusiana na tukio hilo.

Kwa mujibu wa Benjamin, juzi saa 10 hadi saa 12 jioni ulikuwa ndiyo muda wa mwisho kikanuni kwa wagombea kurudisha fomu.

Alisema kabla ya muda huo, watu wa karibu na mgombea mwenza wa Mdede, Moses Madenge, walipanga kukutana ili wakarudishe pamoja fomu.

Hata hivyo, alisema walimsubiri Mdede muda mrefu bila kutokea.

“Baadaye, akawa hapatikani kabisa,” alisema Benjamin alipokuwa akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana.

Alisema kutokana na hali hiyo, alitoa taarifa kwa Mshauri wa Wanafunzi wa Chuo hicho, Mapunda.

Benjamin alisema yeye na Mapunda walianza kazi ya kumtafuta Mdede sehemu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nyumbani kwake, eneo la Nyakato, lakini hawakufanikiwa kumuona.

Hivyo, alisema waliamua kwenda kituo cha polisi kutoa taarifa.

Alisema polisi waliwaeleza kuwa wanachukua maelezo yao kama taarifa tu, lakini hawawezi kuyafanyia kazi mpaka baada ya saa 24.

“Hili tukio linatutatiza sana. Maana hatujui yuko wapi, usalama wake ukoje, ni kina nani waliomkamata au kitu gani kimemsibu,” alisema Benjamin.

Hata hivyo, alisema enzi za uongozi wa Mdede, aliwahi kuwaeleza kuwa alikuwa akipata mashinikizo kutoka kwa watu, ambao hajawataja, wakimtaka atoe tamko kuhusiana na mchakato wa Katiba mpya ya Tanzania.

“Yapo maneno kama hayo, lakini hatuna uhakika nayo. Ila yeye mwenyewe (Mdede) alikuwa anasema. Tuliwahi kumuuliza atueleza ni kina nani waliokuwa wakimpa mashinikizo hayo, kama ni Ukawa au CCM, lakini alitujibu kuwa muda wa kuwataja watu hao bado haujafika,” alisema Benjamin.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alipoulizwa na NIPASHE jana kwa njia ya simu, alisema anawasiliana na watendaji wake kupata taarifa kamili kwa kuwa wakati huo alikuwa bado hajapata taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo.

“Nakuahidi ushirikiano wa hali ya juu,” alisema Kamanda Mlowola na kuahidi kutoa taarifa baadaye, ahadi ambayo hakuitekeleza hadi tunakwenda mitamboni.

Naye Mapunda alipotafutwa jana ili  kueleza hatua gani zinazochukuliwa na chuo chake, alijibu kuwa yupo kwenye kikao hadi tunakwenda mitamboni.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa