Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza,
imemwachia huru mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli (CHADEMA) baada
ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kosa la uchochezi
lililokuwa likimkabili.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Faustine
Kishenyi, alisema kuwa mahakama inamwachia huru mtuhumiwa kwa vile
upande wa Jamhuri haukuweza kuleta ushahidi wa kutosha ambao ungeweza
kuishawishi mahakama imwone ametenda kosa la uchochezi.
Katika hukumu hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi
wengi, hakimu Kishenyi alisema Jeshi la Polisi lilishindwa kuwasilisha
vielelezo mahakamani kama ilivyokuwa katika hati ya mashitaka.
Pamoja na kukosekana kwa vielelezo, upande wa mashitaka pia
ulishindwa kuwasilisha kanda (CD) inayodaiwa kurekodiwa wakati
mshitakiwa akitenda kosa hilo.
Badala yake ni askari polisi watatu waliojitokeza mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya mshitakiwa.
Alisema kutokana na Jamhuri kushindwa kuthibitisha uwepo wa kosa la
uchochezi, mahakama hiyo imejiridhisha kwamba mshitakiwa hakutenda kosa
hilo na inamwachia huru.
Awali ilidaiwa na mwendesha mashitaka wa polisi, Inspekta
Samwel Onyango kuwa Machemli (39) alitoa maneno ya uchochezi
Oktoba 23, 2011 wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji
cha Nyamanga Ukara.
Katika kesi hiyo namba 19, ilidaiwa na upande wa mashitaka kwamba
mbunge huyo kwa makusudi aliwachochea wananchi akiwataka
kuhakikisha wanapambana na polisi na hata kuwashambulia pale
watakapokwenda katika maeneo yao kukamata wahalifu.
Akizungumza mara tu baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Machemli
alidai kuridhika na uamuzi wa mahakama kwa sababu ni wa haki.
“Nimefurahi sana na ninajisikia vizuri kwa sababu kwanza ni kesi
iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na makundi mengi ya watu. Lakini pia
imechukua muda mrefu na imekuwa ikinisumbua kwa wakati wote,”alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment