Tone

Tone
Home » » SERIKALI YAPANIA KUTATUA SHIDA YA MAJI VIJIJINI

SERIKALI YAPANIA KUTATUA SHIDA YA MAJI VIJIJINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Maji,Profesa Jumanne Maghembe.
 
Serikali imedhamiria kufanya mabadiliko makubwa ya kupeleka maji katika maeneo mengi vijijini kati Juni, mwaka huu na mwishoni mwa mwaka 2015.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, (pichani) alisema lengo hilo ni kuhakikisha kwamba serikali inatekeleza Sera ya Maji nchini.

Profesa Maghembe aliyasema hayo jijini Mwanza wakati akizungumzia Sera ya Maji na utekelezaji wake katika kuwafikia wananchi kwenye maeneo ya vijijini na mijini.

“Kupitia wizara ya Maji, serikali imeanzisha miradi mbalimbali ya maji hapa nchini yote ni katika kutekeleza Sera ya Maji ambayo inasema kila mwananchi angalau asiishi umbali wa mita 400 kutoka eneo la maji yanakopatikana,” alisema.

Alifafanua kuwa upatikanaji wa maji nchini ni kwenye miji mikuu ya mikoa na Jiji la Dar es Salaam, vijijini,  miji midogo na miji mikuu ya wilaya.

“Katika miji mikuu ya mikoa na Dar es Salaam, wastani wa upatikanaji wa maji ni asilimia 88 kama ilivyoelezwa kwenye sera ya maji, lakini ziko tofauti kutoka mji mmoja hadi mwingine,” alisema.

Alisema kwa maeneo ya vijijini upatikanaji wa maji ni asilimia 49.

“Tunategemea kwamba mpaka kufikia Juni, mwaka huu tutafika asilimia 55 na kufikia asilimia 74 ifikapo Desemba, mwaka 2015,” alisema.

Alifafanua kuwa katika maeneo ya miji mikuu ya wilaya na miji midogo kama Mombo na miji mikuu kama Muheza, Korogwe, Mwanga, Magu, Lamadi, Chato, Makambako na Tunduru, upatikanaji wa maji ni wastani wa asilimia 51.5.

Alisema lengo la Sera ya Maji ni kufikia mwaka 2015 katika miji midogo maji yawe yamefika kwa asilimia 55.

Aliongeza kuwa hivi sasa wizara yake inatekeleza miradi 1,600 ambapo pamoja na matatizo ambayo wanakumbana nayo ya kifedha, bado miradi mingi imekamilika.

Mapema katika ziara yake mkoani humo, Waziri Maghembe alitoa rai kwa Watanzania kulinda vyanzo vya maji na kuwasihi kutunza miundombinu yake.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa