JUMUIYA
ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Mkoa wa Mwanza imeridhishwa na
ubora wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Ukerewe na
kutaka iwe mfano wa kuigwa na wilaya nyingine nchini.
Pongezi hizo
zilitolewa jana baada ya wajumbe wa jumuiya hiyo kutembelea miradi
mitano yenye thamani ya sh. milioni 693.5 inayotekelezwa katika maeneo
tofauti ya wilaya hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa ALAT tawi la Mwanza,
Henry Matata alisema mbali na miradi ya majengo ya taasisi tofauti
waliyotembelea kuwa katika viwango vya kuridhisha pia barabara zake ni
nzuri na zinapitika.
Akionekana kufurahishwa na uwajibikaji wa
halmashauri hiyo, Matata ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya mji
wa Ilemela, alisema ALAT imetoa mchango wa sh.milioni. 2.1 kuchangia
miradi hiyo.
Kati ya fedha hizo sh. 800,000 zimetolewa kwa kikundi
cha Bure Garden kinachojishughulisha na kilimo na usindikaji mazao huku
kiasi sawa na hicho zikitolewa kukamilisha jengo la kupumzikia wagonjwa
katika Hospitali ya wilaya hiyo na sh. 500,000 zikitolewa kusaidia
ujenzi wa jengo la utawala katika sekondari ya Mumbuga.
Hata hivyo,
alisema jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya
halmashauri kushindwa kuwasilisha michango yake kwa wakati sababu
inayokwamisha mipango ya jumuiya.
Taarifa iliyotolewa katika kikao
hicho inaonyesha hadi kufikia mwaka huu halmashauri sita kati ya saba za
mkoa huo zinadaiwa sh. milioni 84.3 ambapo Ilemela inadaiwa sh. milioni
9 , Kwimba sh. milioni 5, Misungwi sh.milioni 19, Sengerema sh.milioni
8.5, Magu sh. milioni. 18.3 na Ukerewe sh. milioni 17.5.
Mwenyekiti
wa Halmashauri hiyo, Joseph Mkundi, akipokea msaada huo, alisema
halmashauri yake ipo makini na itaendelea kusimamia kwa karibu shughuli
na miradi yote ya umma ili kuiwezesha jamii kupata huduma bora.
Akifafanua
zaidi aliunga mkono utaratibu wa jumuiya hiyo waliojiwekea wa
kutembelea miradi na kufanya vikao kwa kila wilaya kwa maelezo kuwa
unawezesha wajumbe kujifunza mbinu mbadala za maendeleo na kuongeza wigo
wa ufahamu katika kusimamia majukumu yake.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment